Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji Charles Mwijage amesema serikali imemaliza kutayarisha muongozo wa kuondoa kero zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara nchini. Muongozo huo uliopewa jina la Regulatory Reform Blueprint, umeandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa lengo la kuziunganisha mamlaka ya usimamizi na kupunguza muda wa kukamilisha utaratibu wa kisheria kuwekeza.
Ripoti ya Easy of Doing Business 2018 inayotolewa na Benki ya Dunia imeonyesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya 162 kati ya nchi 190 zilizoshiriki katika tathmini ya urahisi wa ufanyaji biashara duniani. Kwa mujibu wa Waziri Mwijage, muongozo ulioandaliwa utasaidia kuondoa vikwazo katika sekta za biashara pamoja na uwekezaji na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi huku akisisitiza hali hii kushughulikiwa ili kuipandisha nchi katika orodha hiyo.