Home BIASHARAUWEKEZAJI TARI yasaini mkataba wa ruzuku Tsh bilioni 2.4

TARI yasaini mkataba wa ruzuku Tsh bilioni 2.4

0 comment 381 views

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imesaini mkataba wa ruzuku ndogo wa jumla ya Kroner ya Norway milioni 9.9 sawa na Tsh. Bilioni 2.4 kwa ajili ya kuendeleza elimu na utafiti kuhusu masuala ya afya ya udongo na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hati hiyo imesainiwa na Ivar H. Kristensen ambae ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi wa Kilimo ya Norway na Dkt. Thomas Nestory, Mkurugenzi Mkuu TARI.

Hati hiyo ni miongoni mwa hati mbili za za makubaliano na mkataba mmoja zilizosainiwa katika ziara ya Kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Norway.

Hati ya kwanza imesainiwa na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Anne Beathe Tvinnereim na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa upande wa Tanzania inayohusu ushirikiano wa usalama wa Chakula na Kilimo.

Hati ya pili imesainiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maisha cha Norway (NMBU) Siri Fjellheim na Prof Raphael Tihelwa Chidunda kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Tanzania (SUA).

Wakati huo huo, Rais Samia ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuunganisha nguvu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochangia uhaba wa chakula katika nchi mbalimbali hususani barani Afrika.

Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula akihitimisha ziara yake ya Kitaifa ya siku mbili nchini Norway.

Rais Samia amesema pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania kwa mwaka 2022/2023 haijakabiliwa na uhaba wa chakula na imefanikiwa kuziuzia nchi jirani tani milioni tano za chakula ili kukabiliana na tatizo hilo.

Mbali na kukutana na Mfalme Harald V, Rais Samia pia ameshiriki Mkutano wa Jukwaa la Nishati la Oslo, amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Norway na pia kukutana na Diaspora kabla ya kuhitimisha ziara yake.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter