Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Tehama Tanzania (ICT) Samson Mwela amesema tume hiyo ipo katika harakati ya kumpata mwekezaji katika viwanda vya mabaki na bidhaa zitokanazo na Tehama. Mwela amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam ambapo amesema kuna fursa mbalimbali kwenye sekta hiyo na uwekezaji unahitajika ili kuleta manufaa kwa nchi. Mwela amefafanua kuwa uwekezaji katika sekta ya Tehama utachochea kasi ya uchumi na viwanda na kusisitiza kuwa tume hiyo kuwavutia wadau wa Tehama kuwekeza zaidi katika sekta hiyo.
“Katika kutekeleza mipango hiyo tume imekuja na mpango wa kuanzishwa kwa viwanda vitokanavyo na mabaki ya bidhaa za kielektroniki ambapo mpango huu umepewa jina la E-waste and Manufacturing Industry”. Amesema Mwele.
Kaimu Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa tume yake imeendesha uchunguzi wa kina ili kufahamu kiasi gani sekta hiyo inaweza kutekeleza ujenzi wa viwanda ili kuiwezesha serikali kutimiza azma ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda mwaka 2025.
“Kwa kuliona hili, sisi kama tume tumekuja na mpango huu ambao utawezesha kuzalisha bidhaa bora na za kisasa zitakazotokana na mabaki ya zana zinazotokana na Tehama”. Ameeleza Mwele.
Mbali na hayo, Kaimu huyo pia amesema mpango huo kwa kiasi kikubwa utasaidia kutunza mazingira kwani mabaki ya zana hizo yatageuka malighafi viwandani ili kuzalisha bidhaa mpya.