Home BIASHARAUWEKEZAJI Unataka kununua kiwanja? Zingatia vitu hivi

Unataka kununua kiwanja? Zingatia vitu hivi

0 comment 192 views

Imekuwa ni kawaida kusikia watu wanataka kuwekeza katika ardhi au viwanja. Uwekezaji katika ardhi ni jambo zuri kwani mbali na kujenga mmiliki ana uwezo wa kuuza kwa fedha nyingi zaidi kutokana na maendeleo yatakayotokea katika eneo husika. Licha ya uwekezaji huu kuwa na manufaa mbalimbali, watu wengi pia wamepata hasara kutokana na kununua ardhi katika namna zisizo sahihi ikiwa ni pamoja na kutofuata sheria na kununua kwa njia zisizo rasmi.

Hivyo basi ni mambo gani ambayo kila mtu anayetaka kuwekeza katika ardhi anatakiwa kuzingatia ili kuepuka hasara? Baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia ni haya yafuatayo;

Hakikisha unamfahamu mmiliki halisi. Watu wengi wamepata changamoto ya kununua ardhi kutoka kwa watu ambao si wamiliki halali. Pia kuna baadhi ya ardhi huwa ni urithi hivyo huwa kunakuwa na wamiliki kadhaa na inaweza kutokea mmoja wa wamiliki akauza ardhi hiyo bila ridhaa ya wengine. Ndio maana inashauriwa kununua ardhi iliyopimwa ili iwe rahisi kujua wamiliki halisi kupitia nyaraka ambazo zimehakikiwa kwa mujibu wa sheria.

Fanya utafiti wa kisheria. Asilimia kubwa ya wanunuzi wamejikuta katika migogoro ya kisheria baada ya kununua ardhi kutokana na kutofanya utafiti wa kutosha. Hivyo hakikisha unajua kila kitu katika upande wa sheria ikiwa ni pamoja na mambo yanayoruhusiwa na yasiyoruhusiwa kufanyika katika eneo husika. Ni muhimu kujua kama ardhi unayotaka kununua inadaiwa au imewekwa rehani. Pia ni muhimu kujua kama ardhi hiyo imetengwa kwa ajili ya matumizi ya kiserikali au la. Mara kadhaa tumeshuduhia watu wakibomolewa nyumba zao au kutakiwa kuhama kutokana na hili.

Huduma za kijamii. Kila mtu hufurahia kupata ardhi kwa gharama nafuu lakini muda mwingine vitu vya bei rahisi vinaweza kukusababishia utumie fedha nyingi zaidi. Kabla hujanunua ardhi hakikisha unazingatia huduma za kijamii zillizopo katika eneo hilo ili kujiepusha na gharama zisizokuwa na umuhimu. Baadhi ya mambo ya kuzingatia ni pamoja na hali ya barabara, ukaribu wa huduma kama hospitali, soko, shule, nk.

Jiografia. Imekuwa kawaida kuona watu wanaathirika na majanga yanayotokea kutokana na mtindo wa kijiografia ulivyo katika maeneo wanayoishi kwa mfano katika eneo la Jangwani, jijini Dar es salaam kila mwaka lazima kuwe na waathirika wa mafuriko na kila mwaka watu hurudi katika eneo hilo na kufanya makazi jambo ambalo si sahihi. Hivyo kama mtu makini unayetaka kuwekeza katika ardhi kwa malengo hakikisha unafahamu jiografia ya eneo ili kujiepusha na majanga ya asili kama mafuriko.

Husisha sheria katika mchakato mzima, mbali na kuwa na mashahidi ni vyema zaidi kuhusisha wataalamu wa masuala ya kisheria ili kuwa katika upande sahihi ikiwa changamoto yeoote itatokea huko mbele. Aidha, hakikisha unapewa nyaraka zote muhimu ili kutambulika kama mmiliki halali.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter