Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amekagua maendeleo ya ujenzi wa viwanda vya Dawa vya Vista Pharma Limited pamoja na Kairuki Pharmaceutical Limited mkoani Pwani.
Waziri Mwalimu mbali na kukagua ujenzi wa viwanda hivyo unavyoendelea, pia amelenga kutatua changamoto ambazo wawekezaji hasa wale wa viwanda vya dawa wanakumbana nazo, ili kuokoa fedha nyingi ambazo hutumika kuagiza dawa nje ya nchi.
“Katika kila Shilingi 100 ambayo serikali inatumia kununua dawa, vifaa na vifaa tiba, Shilingi 94 tunaipeleka nje ya nchi kununua dawa, vifaa na vifaa tiba, na ndio maana nimefanya ziara hii pamoja na viongozi wa mkoa na kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Kituo cha Uwekezaji ili kuokoa fedha hiyo inayopotea nje ya nchi. Dawa kupatikana kwa wingi na kwa bei rahisi na kwa haraka zaidi, kwa sababu kuagiza dawa nje ya nchi MSD anatumia mpaka miezi 6 mpaka ifike Tanzania”. Amesema Waziri huyo.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy amewashukuru wawekezaji hao kwa kuwekeza katika viwanda vya dawa ili kuisaidia watanzania ambao wamekuwa wakipata shida kupata dawa.