Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wawekezaji Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kulipa deni la Sh. 331.2 milioni wanalodaiwa, kwani wasipofanya hivyo serikali itavunja mikataba na wahusika wote watakamatwa na mali zao kutaifishwa.
Mpina amesema hayo alipokuwa akizungumza katika ziara ya kutembelea Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu kwenye Visiwa vya Mbudya na Bongoyo na kusisitiza kuwa, serikali haiwezi kukubali kuchezewa na wawekezaji ambao hawajajipanga kwani wanachelewesha uendelezaji wa fukwe pamoja na maeneo mengine ya urithi wa nchi, na vilevile kukwamisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Katika maelezo yake, Waziri huyo amesema Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu ni utajiri na urithi mkubwa kwa taifa kutokana na fukwe ndefu na nzuri za kipekee duniani, makaburi ya kihistoria, mazalia ya samaki, matumbawe yenye mvuto wa kipekee na ndege ambao hawapatikani maeneo mengine duniani.
Kwa upande wake Meneja wa MPRU, John Komakoma amemueleza Waziri Mpina kuwa maagizo yote yatasimamiwa kikamilifu na kutekelezwa kwa wakati ili taasisi hiyo iweze kuchangia pato la taifa kikamilifu.