Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu amesema Wizara hiyo imejipanga kikamilifu kuwasaidia wawekezaji walio na nia ya kuwekeza kwenye fukwe kwa ajili ya utalii. Kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwaka jana ambapo aliagiza Wizara hiyo kuanzisha Kurugenzi ya fukwe itakayobeba jukumu la kusimamia na kuendeleza fukwe zote nchini, Wizara hiyo imeanza kuyatambua na kuainisha maeneo kwa ajili ya utalii wa fukwe katika kisiwa cha Mafia.
Katika maelezo yake, imeelezwa kuwa, lengo la serikali kuanzisha mkakati huo ni kuhakikisha mapato yanayotokana na sekta ya utalii kupitia utalii wa fukwe yanaongezeka na hivyo kukuza pato la taifa zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaib Nnunduma amesema kuwa wilaya yake inawakaribisha wawekezaji wenye malengo ya kuwekeza mahali hapo huku akiahidi kuwa, atatoa ushirikiano wa kutosha. Nnunduma amesema kuwa wilaya hiyo tayari imeshatenga maeneo maalum ya wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa hoteli za kiutalii katika maeneo ya ufukweni.