Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ernest Mwamwaja amesema bodi hiyo itaanza kuvitangaza vivutio vya mambo ya kale kama jitihada ya kuchochea ukuaji wa idadi ya watalii hapa nchini. Mwamwaja amesema hayo katika ziara ya watendaji wa TTB mkoani Songwe ambapo bodi hiyo mbali na kutembelea kimondo kilichopo Mbozi pia wamepata nafasi ya kufanya mkutano na uongozi wa mkoa huo kuona namna gani wanaweza kukuza utalii kupitia vivutio hivyo.
Mwamwaja amefafanua kuwa rasilimali kama hizo ambazo zinabeba historia ya taifa pamoja na tamaduni mbalimbali ni kivutio kikubwa kwa wageni hivyo kuna kila sababu ya kuvitangaza ili wageni zaidi wapate msukumo wa kuvitembelea.
Ametoa wito kwa wale wanaotoa huduma za kitalii kama vile hoteli, wasafirishaji na hata waongoza watalii kuwa na utaratibu wa kutembelea vivutio vya kale kama vile kimondo cha Mbozi ili kutangaza vivutio hivyo na kuhimiza watalii zaidi kuvitembelea.