Mtandao wa simu unaongoza nchini, Vodacom Tanzania PLC leo imetangaza makubaliano na Google ili kuwapa wateja wake fursa ya kununua maudhui mbali mbali kwenye Google Play store kwa kutumia salio la simu. Huduma hii, ambayo inapatikana kwa wateja wote wa Vodacom wenye vifaa au simu za Android, inawezesha ununuzi wa programu mbali mbali kwenye Google Play Store kwa kutumia salio la simu kwenye mtandao wa Voda.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi huo, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa umma, Bi. Jacquiline Materu alisema: “Kwa kuwa Mtandao wa 4G superfast wa VODACOM una kidhi, tunafurahi kushirikiana na Google kuleta njia hii rahisi, nyepesi na ya kuaminika ya malipo kwenye Google Play Store kwa ajili ya ununuzi wa app ama programu mbali mbali kwa Watanzania. Hii ina imarisha zaidi azimio yetu ya kuzidi kuwakaribisha wateja wetu katika ulimwengu wa kidijitali huku tukiwapatia urahisi na thamani kutokana na matumizi ya kadi za benki kwa ajili ya kufanya manunuzi mtandaoni kuwa mdogo sana hapa nchini.
Sasa wateja wa Vodacom wenye vifaa ama simu za Android wanaweza kununua maudhui katika Google Play Store, kama programu, michezo, muziki, filamu, maonyesho ya TV na vitabu vya kielektroniki kwa urahisi zaidi, kwa kutumia salio la simu kwenye mtandao wa Voda. Hapo awali ni kadi za benki tu ndizo zilikuwa zikitumika kufanya manunuzi hayo.
Materu aliendelea kufafanua kuwa, uvumbuzi huu utarahisisha mchakato wa malipo na kuboresha huduma kwa wateja wake.
“kama jukwaa la kuwasilisha maudhui, tunabeba jukumu la kutaarifu, kuelimisha na kuburudisha wateja wetu kwa kutumia tekinolojia. Aliongeza kuwa, wamepiga hatua kubwa kwa kuwezesha jukwaa mbali mbali za kidijitali na kijamii kuweza kupatikana kirahisi zaidi kwenye mtandao huku wakitengeneza mifumo ya kidijitali yenye kujumuisha kila mtu”
Pembeni yake Cassandra Mensah-Abrampah, Meneja wa Ushirikiano wa Jukwaa la Android | Afrika kutoka Google, alisema, “Tumefurahi sana kuongeza wigo wa ushirikiano wa malipo ya moja kwa moja baina ya Google Play Direct na Vodacom Group ikiwa ni pamoja na kufanya uzinduzi huu na Vodacom Tanzania. Utozaji kwa njia ya simu ni mojawapo ya nguzo muhimu kwenye ujumuishi wa kifedha katika uchumi wa app ama programu katika masoko kwa sababu watu wengi bado hawana akaunti za benki.”
Wateja watakaopenda kutumia njia hii bora ya malipo wanahitaji kufanya ifuatavyo: Ingia kwenye Google Play Store > Chagua content (Games/Apps or Movies) nenda kwenye Buy option > kisha chagua Vodacom Airtime billing as mode of payment, kisha utahitajika kuingiza taarifa zako binafsi na kuendelea na malipo baada ya kuthibitishwa. Hatua hizi zinahitajika tu kwa ununuzi wa kwanza tu. Malipo mengine yote yatakuwa ni ya moja kwa moja baada ya kuchagua mfumo wa malipo wa kutumia salio la simu kwenye mtandao wa Voda.