Biashara ni sekta muhimu kwa nchi yoyote ile katika kuchangia uchumi wa nchi. Hakuna nchi ambayo itaendelea bila ya kuwa sekta imara ya biashara. Lakini ili sekta hii ikomae lazima wafanyabiashara na serikali washirikiane ili kujenga mazingira mazuri ya biashara. Mojawapo kati ya changamoto kubwa katika sekta hii ni kodi.
Wakati Wizara ya Fedha na Mipango ikiwasilisha bajeti yake bungeni mwaka jana, Dk. Philip Mpango ambaye ndiye Waziri katika kitengo hicho cha serikali alisema kuwa jumla ya biashara zilizofungwa hadi kufikia Juni 2017 ni 2,700. Alisema katika maelezo yake kuwa serikali haipaswi kulalamikiwa kutokana ha hali hiyo kwa kuwa wafanyabiashara wengi wemeshindwa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zilizopo.
Wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia tozo za kodi na kulaumu kuwa zinakuwa kubwa kuliko faida wanayoingiza hivyo hali hiyo imepelekwa wengi kufunga biashara zao na kutokomea huku wakiacha nyuma madeni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka hiyo wamekuwa na tabia ya kuwatoza kodi wafanyabiashara katika njia ambayo inawakosesha amani kwa kuwa hawafuati taratibu ambazo mamlaka hiyo imejiwekea hali ambayo wafanyabishara wengi wamekuwa wakiona kama ni uonevu wa wanyonge, jambo ambalo linawavunja moyo katika shughuli zao. Watumishi wachache wanaoharibu taswira ya TRA wanapaswa kuchukuliwa hatua na kuvuliwa jukumu hilo mara moja.
Serikali inawajibu wa kuandaa programu maalum ambayo itaruhusu wafanyabiashara kukutana nao mara kwa mara hivyo kuwapa fursa ya kujadili changamoto zinazowakabili moja kwa moja ili kuonyesha kuwa serikali ina nia njema na sekta hiyo na lengo la wafanyabiashara hao pamoja na serikali ni moja.
Nchi yetu inatakiwa kuondokana na hali hii ya biashara zaidi kufungwa. Kufungwa kwa biashara hizi kunaathiri watu wengine ambao labda walikuwa wakijiingizia kipato halali hivyo hali hii haipelekei kudorora kwa uchumi kwa serikali na wafanyabiashara tu, bali athari zinaelekezwa kwa jamii yote kwa namna moja au nyingine