Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa Maalum wa Kikodi Kahama, Faustine Kayombo amesema baadhi ya wafanyabiashara wilayani humo wamekuwa wakiiandikia mamlaka hiyo barua za kuomba kuacha kufanya biashara na badala yake, kuingia katika mfumo wa vitambulisho vya wajasiriamali maalum kwa ajili ya biashara ndogondogo.
Kayombo amewambia waandishi wa habari kuwa takribani wafanyabiashara 100 tayari wamewasilisha barua zao TRA na baada ya ukaguzi, wamejiridhisha kuwa kuna ambao hawana sifa za kuingizwa kwenye mfumo wa vitambulisho vya ujasiriamali vilivyotolewa na Rais Magufuli.
“Kuna barua nyingi tayari ofisini kwangu na ninapokea idadi ya barua nane hadi kumi kwa siku kutoka kwa wafanyabiashara za kuacha biashara zao, na ofisi yangu imebaini kuwa wengi wao wanakuwa na nia ya kukwepa kulipa kodi na kujiunga na vitambulisho vya wajasiriamali. Mpaka sasa Mamlaka imefanya msako na kujiridhisha na hali hiyo na tuliwabaini wafanyabiashara wawili ambao wana vitambulisho vya wajasiriamali wadogo na tulifanikiwa kuwakamata na kuvinyang’anya na kuvirudisha kwa Mkuu wa Wilaya Anamringi Macha”. Ameeleza Kaimu huyo.
Kayombo ametoa wito kwa walio na sifa za kulipa kodi kuendelea kufanya hivyo huku akiwataka kufika ofisi za TRA na kukadiriwa kodi upya ikitokea mitaji yao inayumba.