Siku chache baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza msamaha wa riba pamoja na adhabu kwenye malimbikizo ya kodi, mamia ya wafanyabiashara wameendelea kujitokeza katika ofisi za mamlaka hiyo na kuomba kuzungumza na wahusika kuhusu kupunguziwa riba. Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa mamlaka huyo Richard Kayombo amesema wafanyabiashara wengi wanazidi kumiminika katika ofisi za TRA kutokana na nafuu iliyotolewa.
Hivi karibuni, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere alitangaza kwa umma kuwa, mamlaka hiyo imepewa uwezo wa kusamehe wafanyabiashara wenye malimbikizo ya madeni kwa asilimia 100. Hapo awali, TRA ilikuwa na mamlaka ya kisheria ya kusamehe madeni kwa asilimia 50 pekee lakini baada ya Bunge kupitia upya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 na sehemu ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kutoa utaratibu maalum wa kumwezesha Kamishna Mkuu kutoa msamaha wa riba na adhabu hadi asilimia 100.