Wito umetolewa kwa watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kwenye ujenzi wa reli ya mwendo kasi inayojengwa kutoka Mwanza kwenda Isaka mkoani Shinyanga itakaogharimu takribani Sh Trilion 3.
Wito huo umetolewa kwenye Kongamano la Mpango Kazi na Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya tano uliokutanisha wadau mbalimbali jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Masanja Kadogosa alisema makampuni yenye sifa yanatakiwa kuomba tenda za aina mbalimbali zinazohitajika kwenye Mradi huo haraka ili kuepuka udanganyifu kwenye shughuli hiyo.
Mhandisi Kadogosa alisema “ujenzi wa sehemu ya Reli SGR toka Mwanza hadi Isaka utagharimu trilioni 3 na utakamilika ndani ya miezi 36 utasaida kuongeza huduma za usafiri kwa wananchi pamoja na bidhaa hivyo kusukuma gurudumu la maendeleo.
Alisema Mradi huo utazalisha zabuni mbalimbali ikiwemo za usafirishaji, ukandarasi, na utatoa ajira za moja kwa moja kwa watu 15,000 na zisizo rasmi 75,000 na itakuwa na urefu wa kilometa 341.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, alisema kukamilika kwa ujenzi wa Mradi huo utasaida wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kutoka na kwenda Dar es salaam kwani zaidi asilimia 80 ya wafanyabiashara hutumia njia hiyo.
Mongella amewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa zitakazoletwa na ujenzi wa Mradi huo kwani utazalisha uhitaji wa huduma nyingi toka kwa watanzania panapopita reli hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliwapongeza TRC kwa kuamua kuzishirikisha taasisi za fedha kuelekea kuanza kwa awamu ya tano ya ujenzi wa SGR kutoka mwanza hadi Isaka.
“Sote tunafahamu, CRDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo, hivyo tutahakikisha tunashiriki kwa njia mbalimbali katika ujenzi wa SGR ikiwemo kutoa mikopo kwa wakandarasi na kufadhili miradi mingine wakati wa ujenzi wa reli,” alisema Nsekela.
Alisema mpaka sasa benki ya CRDB imeweka sera wezeshi kwa wakandarasi ambapo inatoa dhamana ya Bid Guarantee kwa wakandarasi wanaotafuta kandarasi, dhamana ya utekelezaji wa mradi inayofahamika kama Performance Guarantee na dhamana ya malipo ya awali yaani Advance Payment Guarantee.
Afisa Mahusiano wa Benki ya NBC Mwanza, Ester Kahabi amewataka wananchi kuchangamkia fursa za ujenzi wa kipande cha Reli hiyo kwa kuchukua mikopo yenye riba nafuu na kuwekeza katika Miradi ya ujenzi wa reli hiyo.