TAASISI ya New Face Creatives imeipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa namna ambavyo imefanikisha Sera ya elimu bure kwani imeongeza uandikishwaji wa wanafunzi hasa kutoka katika kaya maskini.
Akizungumza jijini Dodoma Mtendaji wa Taasisi hiyo, Mary Mtega amesema mafanikio ya awamu ya tano yamefikia hatua kubwa na kuwakomboa watanzania wengi hasa kaya nyingi zenye kipato kidogo na uhitaji mkubwa wa elimu kwa ngazi ya Shule za Msingi na Sekondari.
Amesema kupitia taasisi yao wameanzisha kampeni ya usambazaji na ugawaji wa madaftari kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum lengo likiwa kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli za kuwapatia elimu bila malipo watoto wa kitanzania.
” Sisi kama taasisi ya kizalendo tumeona tuandae kampeni hii ya usambazaji madaftari ambayo yatakua na picha za Marais na Viongozi wa kitaifa wa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wapo wanafunzi ambao wanamsikia Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere wengine wanamsikia Rais Magufuli lakini hawawajui, sasa sisi kupitia kampeni hii tutagawa madaftari yenye picha za viongozi wetu wa bara na visiwani,” Amesema Mtega.
Ameiomba serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kuwaunga mkono katika kampeni hiyo kwa kuwachangia ili waweze kufanikisha mradi huo wenye lengo la kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli katika Sera yake ya elimu bila malipo.