Bima ya afya ni nini?
Bima ya afya ni mfumo wa kujiunga kwa hiari ama kwa lazima unaomhakikishia mwanachama kugharamiwa gharama zinazojitokeza katika kupata huduma za kiafya zikiwemo kumwona daktari, kufanya vipimo pamoja na kupata matibabu na dawa kwa mwanachama husika.
Bima ya afya ni kama mkataba unaoingiwa na anayetaka huduma pamoja na mtoa huduma kwa kupitia mifuko au taasisi inayowaunganisha mtoa huduma pamoja na mhitaji wa huduma husika.
Mara nyingi Bima ya afya hujumuishwa kwenye makato anayoyatoa mwajiri kwa waajiriwa wake katika kufanya malipo.
Pia zipo bima zinazowahusu watu binafsi, wazee na wasiojiweza, wajawazito na wengine wenye mahitaji maalumu bila kusahau wanafunzi kipindi cha masomo yao.
Mara nyingi wanachama huchagua taasisi ama mifuko inayotoa bima hizi kulingana na aina, viwango na mipaka (coverage) ya Taasisi/Bima hizo.
Ni ukweli uliowazi kuwa kila mfuko huweza kutofautiana na mingine katika huduma inazozitoa kwa mfano kwa hapa Tanzania mfuko wa NHIF (National Health Insurance Fund) ni mfuko unaotumiwa zaidi na wafanyakazi waliopo katika taasisi rasmi wengi wao wakitoka serikalini.
Kwa upande mwingine kuna mifuko mingine tofauti na NHIF kama STRATEGIS, AAR, METROPOLITAN na mingineyo ambayo inafuata utaratibu ule ule wa wafanyakazi wa serikali au wa sekta binafsi kujiunga na mwajiri kuwakata kiwango fulani cha pesa ili kufanya malipo ya kupata uhakika wa matibabu wao na familia zao.
Kwa mantiki hiyo, ni vyema kwa kila mwanachama kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu huduma, viwango na mipaka (limitations) ya mfuko wa bima anaoamua kuuchagua.
Mkombozi wakati wa dharura Bima ya afya ni miongoni mwa bima muhimu sana kwani kuwa nayo hukusaidia kupata matibabu hata kama hauna fedha taslimu.
Hata kama umepata dharura na wasamaria wema wamekusaidia tu kukupeleka hospitali basi wakitoa kadi yako ya bima utatibiwa mpaka utakapopona kulingana na bima yako, hakutakuwa na sababu ya kuchelewesha matibabu.
Hivyo ni muhimu sana kuwa na bima ya afya maana itakusaidia hususani wakati wa dharura ama wakati hali yako ya kifedha sio nzuri.
Hata hivyo kama bima zilivyo ni vyema kujiandaa na kuwa tayari kwani huwezi kujua lini wewe au mtegemezi kutoka kwenye familia yako ataugua.
Bima ya afya husaidia sana pia kukuwezesha kupata matibabu ya gharama kubwa kuliko ile ambayo ungeweza kulipia na huondoa wasiwasi wa gharama za matibabu.
Hivyo basi ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.