Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa kampuni zinazoshughulika na masuala ya bima kutoa huduma hiyo kwa wakulima ili nchi ifanikishe lengo la kufikia uchumi wa kati. Dk. Kijaji ametoa ushauri huo jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa 41 wa Umoja wa kikanda wa kampuni za bima za nchi za mashariki na kusini mwa Afrika (OESAI).
Dk Kijaji amebainisha kuwa takribani asilimia 75 ya watanzania ni wakulima na wengi hawana elimu juu ya bima ikiwemo kupata mikopo ya bei nafuu itakayowawezesha kutatua changamoto za kilimo na kufikia malengo. Naibu Waziri huyo amezitaka kampuni za bima nchini kuangalia kundi hilo la wakulima, ili nao wanufaike kupitia bidhaa wanazozalisha, kwa kuwa kundi hilo ni kubwa na ni fursa kwa kampuni hizo kuongeza idadi ya watumiaji wa bima.
Naye Kamishna wa bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (Tira) Dk. Baghayo Saqware amesema kufanyika kwa mkutano huo hapa nchini ni nafasi nzuri kwa kampuni za bima kujifunza jinsi kampuni za nje zinavyofanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo, Khamis Suleiman amedai lengo kubwa la mkutano huo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya watanzania wanakuwa wamiliki wa aina yoyote ya bima. Hivi sasa Tanzania inashika nafasi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki kwa huduma za bima.