Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya DCB Godfrey Ndalahwa amesema benki hiyo imeanza rasmi kuuza hisa zake kwa wanahisa wa sasa na watanzania kwa ujumla. Akizungumzia uuzaji wa hisa hizo Ndalahwa amesema fursa hiyo ni ya kipekee na watanzania wote wanatakiwa kuichangamkia kwani hisa moja itauzwa kwa bei ya Sh. 265, ikiwa ni bei ya chini kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).
“Dhana kubwa ni kuwaruhusu wanahisa waliopo kununua hisa na kutoa nafasi kwa wawekezaji wengine kununua hisa zitakazobaki. Uuzaji hisa za DCB umegawanywa katika awamu mbili, awamu ya kwanza itaanza leo hadi Desemba 3, 2018, ambapo hisa zitauzwa kwa wanahisa waliopo katika daftari la wanahisa. Aidha, kuanzia Desemba 4 hadi Desemba 18, 2018, hisa zote zitakazobaki zitauzwa kwa wanahisa waliopo na kwa wawekezaji wengine wasio wanahisa wa DCB. Kwa sasa, daftari limefungwa na mauzo ya hisa za DCB zilizopo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) yamesimamishwa kuanzia November 7 kupisha uuzaji wa hisa”. Amesema Ndalahwa.
Kuhusu utaratibu wa kushiriki, imeelezwa kuwa wanahisa watakaoshiriki ni walioorodheshwa katika rejista ya wanahisa baada ya jalada kufungwa ili kupata idadi ya hisa huku akisisitiza kuwa mwanahisa ana haki ya kununua hisa moja kwa kila hisa mbili anazomiliki.