Gharama za mara kwa mara za uchapishaji wa noti kwa ajili ya kubadilisha picha za viongozi baada ya muda wao wa kuwa madarakani kukoma ndio sababu iliyofanya picha hizo ziondolewe kwenye sarafu ya Tanzania.
Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande ameeleza hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Angelina Adam Malembeka, aliyetaka kufahamu wakati ambao Serikali itabadili mwonekano wa noti na sarafu ili kutoa fursa ya kuweka picha ya Rais Mwanamke wa kwanza Tanzania.
Chande amesema kuwa uamuzi wa kuondoa picha ya Rais kwenye noti ulifanyika katika kipindi cha Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa, kuanzia toleo la noti la mwaka 1997 ambapo picha ya Kiongozi wa nchi iliondolewa.
Amesema kuwa picha hiyo iliondolewa na badala yake ikawekwa picha za wanyama kama vile Tembo kwenye noti ya shilingi 10,000, Kifaru kwenye noti ya shilingi 5,000 na Simba kwenye noti ya shilingi 2,000 ili kuondoa gharama za mara kwa mara za uchapishaji wa noti.
Aidha, ameeleza kuwa katika kuenzi michango ya waasisi wa Taifa la Tanzania, noti ya shilingi 1,000 imeendelea kuchapishwa ikiwa na picha ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na noti ya shilingi 500 ilichapichwa ikiwa na picha ya Rais wa awamu ya kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Hata hivyo ameongeza kuwa, noti ya shilingi 500 ilibadilishwa kuwa sarafu mwaka 2014 ambapo picha ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume imeendelea kuwepo.