Na Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) kufanya kazi bila hofu ili Tanzania iwe nchi isiyo na rushwa hali itakayopelekea maendeleo kuwafikia wananchi wa kawaida. Ameagiza Taasisi hiyo kukamata wote wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa ili kusudi sheria ichukue mkondo wake.
Rais Magufuli amesema hayo Ikulu jijini Dar es salaam jana katika hafla ya kumuapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru. Ameongeza kuwa tatizo la rushwa likifanikiwa kupungua hapa nchini, matatizo mengi yatatatuliwa. Rais amesema kuwa vita hii dhidi ya rushwa inayoendelea imeanza kuvutia wafadhili na wawekezaji wengi zaidi kufika hapa nchini.
Kwenye hafla hiyo pia, Rais aliipongeza Takukuru kwa kazi nzuri wanayofanya na kuitaka kuendelea na kasi hiyo ili vita hii dhidi ya rushwa izae matunda ambayo yataonekana. Ameeleza kuwa yeye kama kiongozi atapambana na tatizo hili kiukweli na ameomba wananchi nao kushirikana ili kumaliza adha hii ya rushwa katika maeneo mbalimbali ya kazi.