Home FEDHA Magufuli arejesha kikokotoo cha zamani, Mkurugenzi SSRA atumbuliwa

Magufuli arejesha kikokotoo cha zamani, Mkurugenzi SSRA atumbuliwa

0 comment 108 views

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameagiza vikokotoo vya zamani vya mafao ya wafanyakazi wa serikali pamoja na sekta binafsi katika mifuko ya hifadhi ya jamii viendelee kutumika kwa kila mfuko hadi mwaka 2023. Rais Magufuli ametoa uamuzi huo alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), vyama shiriki, watendaji wakuu wa mifuko ya Hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa ajili ya kujadili kwa pamoja mjadala wa kikokotoo kipya cha mafao kwa wastaafu.

Rais Magufuli ameagiza utaratibu wa zamani kuendelea kutumika ambapo wastaafu watapatiwa mafao ya mkupuo ya asilimia 50 kwa wastaafu wa serikali na asilimia 25 kwa wale wa sekta binafsi na sio kama ilivyopendekezwa katika kanuni mpya za ukokotoaji.

“Mstaafu anaambiwa fedha nyingine atunziwe ili aendelee kuishi nazo katika kipindi cha maisha yake. Wanaopanga hivyo wamejuaje kama mhusika anataka kuishi wakati fedha zake anaziona zinavyotumika katika miradi isiyo na tija? Ukweli kabisa tufikirie haya mambo tunayotakiwa kuyafanya ungefanyiwa wewe ingekuaje? Hiki ndicho kitu cha msingi tunachotakiwa kukibeba”. Ameeleza Rais Magufuli.

Aidha, baada ya kufanyika kwa kikao hicho na Rais, taarifa iliyotolewa na Ikulu imeeleza kuwa Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa SSRA Dk. Irene Isaka. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu mpya utafanywa baadae.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter