Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ametoa wito kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuja ya mbinu mbadala ili kuwainua wakulima wadogo wa kahawa kwa njia ya mikopo, ili nao waweze kujikwamua kupitia kilimo wanachofanya na kubadili maisha yao. Gaguti amesema baada ya benki hiyo kuviwezesha vyama vya msingi vya ushirika, ni muda muafaka wa TADB kuangalia jinsi gani wanaweza kutoa mikopo nafuu moja kwa moja kwa wakulima wadogo.
“Pamoja na benki hiyo kutoa mikopo kupitia vyama vya ushirika, ni vizuri kungekuwa na utaratibu mwingine wa kuwasaidia wakulima wadogo ili kuwajengea uwezo zaidi wa kuzalisha zao hilo. Nitoe ombi kwa TADB kufikiria uwezekano wa kutoa mikopo nafuu kwa wakulima mmoja mmoja au vikundi ambavyo vitawaongezea tija. Nimepata fursa ya kuwatembelea baadhi ya wakulima wa kahawa mkoani hapa, nimeona wanayo maono mapana ya kukuza kilimo chao kuwa cha kisasa zaidi”. Ameeleza Mkuu huyo.
Katika maelezo yake, Gaguti amesema tayari mabadiliko makubwa yameanza kuonekana mkoani Kagera baada ya serikali kushirikiana na TADB kuleta mfumo mpya wa namna ya kusimamia soko la zao la kahawa. Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Japhet Justine amesema benki hiyo inalenga kuinua sekta ya kilimo hapa nchini ikiwa ni mchango stahiki katika kuimarisha uchumi wa taifa.