Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Dodoma Rehema Chuma amewataka wakulima pamoja na wajasiriamali kujiunga katika vikundi kupata fursa za mikopo inayotolewa na shirika hilo. Meneja huyo ametoa wito huo alipokuwa katika maonyesho ya nanenane ambayo mkoani humo yalifanyika katika viwanja vya Nzuguni. Chuma ameeleza kuwa, wajasiriamali na wakulima wakiunda vikundi vyao, watakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kupatiwa mikopo na NSSF.
“Hatuwezi kumsaidia mtu mmoja mmoja, wanatakiwa kujiunga kwenye vikundi ili kuwa rahisi kutambua na kuwawezesha na fursa ya mikopo tunayotoa”. Amedai Chuma.
Meneja huyo amefafanua kuwa mikopo hiyo haitolewi moja kwa moja na shirika la NSSF bali, wameingia mkataba na benki mbalimbali za biashara kati ya hizo zikiwemo NMB na Azania. Pia amesema kuwa makundi ambayo ndio walengwa wakubwa wa mikopo hiyo ni pamoja na wajasiriamali, wavuvi, wakulima, waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja na mamalishe (wauza chakula) huku akisisitiza kuwa walengwa wote wanatakiwa kuwa wamejiunga na vikundi rasmi vya uzalishaji mali kama Amcos, Saccos, Vicoba na Vibindo.