Wananchi wametakiwa kukopa mikopo inayotolewa na Serikali na Taasisi rasmi ili kujiepusha na udhalilishaji unaoweza kutokea kutokana na kukopa mikopo yenye masharti magumu kutoka kwa Taasisi zisizo rasmi na kwa wakopeshaji binafsi.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Binuru Shekidele alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambayo ipo mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
Aliongeza kuwa mikopo rasmi inayotolewa na Serikali na Taasisi zilizoidhinishwa hufuata taratibu za kisheria ambazo zinalinda haki za wakopaji na kuhakikisha wanapata huduma za kifedha kwa masharti nafuu.
“Mikopo rasmi kutoka serikalini ina masharti nafuu, riba ya chini, na inalenga kuwawezesha wananchi kuboresha maisha yao bila kuingia kwenye matatizo ya kifedha,” alisema Shekidele.
Alifafanua kuwa ni muhimu kwa wananchi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masharti ya mikopo wanayochukua ili kuhakikisha wanakopa kwa uangalifu na kulipa kwa wakati bila kuingia katika changamoto zisizo za lazima.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Jacob Nkungu aliwashauri watoa huduma za fedha kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi bila kuwakandamiza.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha mkazi wa Sengerema, Boniface Maxmilian, alishauri elimu ya fedha ifike kwa wananchi wote katika ngazi zote ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo kufahamu mikopo salama, kuwa na uelewa wa masuala ya bajeti na kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Naye Afisa Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Santley Kibakaya alisema kuwa baada ya kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali wananchi watabadilisha utaratibu wa maisha, ikiwemo kuacha kukopa kwenye Taasisi ambazo sio rasmi, kuwashirikisha wenza wao kabla ya kuchukua mikopo na kutotumia mali za familia kama dhamana ya mkopo bila ridhaa ya wanafamilia.