Serikali imewashauri wananchi kusajili vikundi vyao vya huduma ndogo za fedha kupitia mfumo wa Wezesha Portal ambayo ni njia rahisi na haina gharama yoyote.
Ushauri huo umetolewa na, Afisa Usimamizi Fedha Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Jackson Mshumba wakati akitoa Elimu ya Huduma Ndogo za Fedha katika Kata ya Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro.
Mshumba amesema kuwa Wezesha Portal ni jukwaa la dijitali lililoundwa kusaidia wajasiriamali na wafanyabiashara katika kukuza biashara zao, kupata mafunzo, na kupata rasilimali zingine za kuwasaidia kibiashara na inaokoa muda.
Aidha, amesema kuwa kabla ya kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha ni vyema wananchi wanaotaka kuanzisha vikundi hivyo wakajiridhisha kuhusu wanachama wao wanaotaka kujiunga nao ili kuepukana na lawama na baadhi ya wajumbe kukimbia familia zao kutokana na madeni.
“Kabla ya kujiunga kwenye kikundi kitu cha kwanza lazima wawe wanatoka eneo moja ili kurahisisha utambuzi katika Serikali za Mitaa, pili, lazima waaminiane, tatu, wawe na lengo moja lililosababisha wao waamue kuanzisha kikundi,” amesema Mshumba.