Kila mtu ana malengo ambayo anatamani kuyafanikisha. Fedha ni kiini cha kuyafanikisha malengo hayo. Kwasababu bila fedha huwezi kununua gari unayoipenda, kujenga nyumba itakayokidhi mahitaji yako, au kufungua biashara ambayo umekuwa ukitamani kuifungua. Hivyo basi ili kutimiza malengo ni lazima katika kipato unachopata uwe na mazoea ya kujiwekea akiba. Zifuatazo ni njia salama za kuhifadhi fedha za akiba:
1. Benki
Kuna aina kadhaa za akaunti katika mabenki. Hivyo ni muhimu ukiwa unataka kuweka akiba uamue unataka kuweka fedha zako katika mfumo gani. Kuna wale ambao huwa na akaunti ambazo wanakuwa wanaweza kutoa fedha zao muda wowote, na kuwa wale ambao huwa na akaunti ambazo huruhusiwa kutoa fedha kwa kikomo fulani kwa mwezi (hii ni nzuri kwa wale ambao hawana matumizi mazuri ), na kuna wale ambao huwa na akaunti ambazo huweka fedha kwa muda mrefu na hukubaliana na sharti la kutotoa fedha hizo baada ya miaka kadhaa ( Fixed account). Hivyo kulingana na matumizi yako unaweza kuamua ni aina ipi ya akaunti itakufaa kwasababu lengo ni kuhakikisha unakuwa na akiba ambayo itakusaidia kufanya shughuli za kimaendeleo. Na kwa ujumla benki ni sehemu salama sana kwa ajili ya kujiwekea akiba ili mradi muhusika akikidhi masharti na vigezo vya kumiliki akaunti katika benki husika.
2. Kuwekeza katika biashara
Mtu yeyote akiwa na fedha za akiba siku zote hutaka kuzitumia fedha hizo kwenye kila jambo hata yale mambo yasiyokuwa na msingi. Hivyo basi ili kuwekeza akiba yako na kuifanya akiba hivyo iongezeke si vibaya kama ukiwekeza fedha hivyo kwenye biashara, na muda mwingine si lazima uwekeze katika biashara yako kwasabu si kila mtu ana kipawa cha kufanya biashara, hivyo unaweza kuwekeza katika biashara za watu wengine ili mradi kuwepo na makubaliano na mikataba ili uzulumaji usitokee.
3. Kuwekeza katika mali zisizohamishika
Kuna biashara ambazo humpa mfanyabiashara faida za hapo kwa papo na kuna zile ambazo mtu hupata faida baada ya miaka mitano, au kumi ijayo kwamfano kwenye viwanja, mashamba, nyumba, na kadhalika. Hivyo ili kuhakikisha akiba ya fedha yako iko salama unaweza kufanya aina hii ya uwekezaji kwasababu vitu kama ardhi vina dhamani sana. Hasa kwasababu watu wanaendelea kuongezeka duniani hivyo uhitaji wa ardhi pia unakuwa mkubwa. Leo unaweza kununua ardhi kwa laki mbili lakini baada ya miaka kumi mbele ardhi hiyo ya laki mbili unaweza kuiuza kwa milioni arobaini na kufanya uwekezaji katika maeneo mengine ambayo yanafaida zaidi kwa kipindi hicho.
4. Ununuzi wa hisa
Hii ni njia moja wapo ya kutunza fedha yenye uhakika wa faida. Kwasababu mfanyabiashara atakuwa na uhakika wa usalama wa fedha zake na uhakika wa faida ambayo hutokana na gawio la mwaka au zaidi inategemea na makubaliano na taasisi ya kifedha husika.
Kwa Tanzania mfanyabiashara au mwananchi yeyote anaweza kununua hisa katika makampuni yaliyojisajili kwenye soko la Hisa lililopo Jijini Dar es Salaam (DSE).
5. Kuweka kwenye vikundi
Kuna aina nyingi za vikudi ambavyo huundwa kwa dhumuni la kuhifadhi fedha ili kuwawezesha wanakikundi kupata maendeleo. Vipo ambavyo huundwa na taasisi za kifedha na vipo ambavyo huundwa na watu binafsi kwamfano marafiki. Hivyo tathmini malengo yako ya kujiunga katika kikundi husika na jinsi utakavyonufaika halafu anza kuhifadhi fedha zako huku ukiwa unajua fedha hizo unawekeza kwasabu ya kutimiza malengo yapi. Kwasabu lengo ni kunufaika na akiba yako kimaendeleo na kuliongezea pato taifa.