Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema hana taarifa yoyote kuhusu taasisi ambayo imetishia kusitisha mkopo au msaada kwa Tanzania kufuatia taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Dk. Mpango amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wakichangia Azimio la Bunge la Mkataba wa Takwimu Afrika.
“Kulikuwa na madai kuwa baadhi ya wadau wametishia kutoa fedha, mimi ndiyo Waziri wa Fedha na sijaona taarifa yoyote ya taasisi iliyoonyesha kuacha kutoa mkopo. Kuna taratibu za taasisi hizi kutoa taarifa na kote sijaona. Kuna taarifa pia kuwa mimi nililegeza masharti ya Sheria hii nilipokutana na watu wa Benki ya Dunia. Ukweli ni kwamba, mimi siwezi kulegeza Sheria iliyopitishwa na Bunge, nilipokutana na Makamu Rais wa Benki ya Dunia nchini Indonesia nilimfafanulia malengo ya Sheria hiyo na nikamwambia kama anaweza kutuma mwakilishi wao wakati tunatunga kanuni za Sheria hii”. Amefafanua Dk. Mpango.
Akieleza kuhusu hoja ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutotoa taarifa za fedha kwa wakati, Waziri huyo amesema kuwa taarifa hizo hutolewa kwa wakati isipokuwa pale kunapokuwa na sababu maalum.