Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sera na mipango yake kwa kuhakikisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo sekta za elimu na afya zinapewa kipaumbele katika Bajeti ya Serikali.
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akifunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Vikao hivyo vimefunguliwa baada ya kukamilisha tathimini ya awamu ya tatu ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility- (ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na maombi mapya ya Serikali ya kupata fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) kutoka Shirika hilo.
Naye, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema Benki Kuu imejitahidi kwa kiasi kikubwa kutekeleza mapendekezo ya IMF kupitia utekelezaji wa sera ya fedha na usimamizi wa sekta ya fedha na Uchumi kiujumla.
Pia, ameahidi kuendeleza ushirikiano na shirika hilo ambao una tija katika ukuaji wa Uchumi wa nchi, ustahimilivu wa bei na ustawi wa sekta ya fedha.
Kwa upande wake, kiongozi wa timu ya wataalamu wa IMF Harris Charalambos Tsangarides, amesema kuwa tathimini yao ya awamu ya tatu imeonesha kuwa Tanzania imetekeleza vizuri mpango wa ECF na kushauri hatua kadhaa zinazotakiwa kuendelea kuchukuliwa.
Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha zaidi huduma za jamii, kusimamia kikamilifu soko la fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania imefanyiwa Tathimini ya Awamu ya Tatu ili iweze kupata fedha kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo hadi sasa imepokea kiasi cha dola za Marekani milioni 455.3 kati ya dola za Marekani bilioni 1.1 ambazo Tanzania itanufaika nazo katika kipindi cha utekelezaji wa program ya ECF.
Aidha, iwapo mapendekezo ya Serikali ya programı mpya ya RSF yataridhiwa na Bodi ya IMF, Tanzania itaongezewa fedha za mkopo nafuu ambazo zitatolewa kwa kıpindi cha miaka miwili (2025/2026).