Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapaswa kujiuliza kwanini wafanyabiashara wengi wanakwepa kulipa kodi na badala yake waamua kuwatumia wamachinga na wafanyabiashara wadogo kuuza bidhaa zao. Rais Magufuli amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa kuboresha majisafi na majitaka katika kijiji cha Kimnyaki jijini Arusha ambapo amesema kuwa, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakikwepa kodi kwa kuwatumia wafanyabiashara wadogo.
“Mnaweka viwango vikubwa ambavyo havilipiki jambo ambalo linafanya wafanyabiashara kukwepa, hivyo ni bora kuweka viwango vidogo vinavyolipika na wengi kuliko kiwango kikubwa kinacholipwa na watu wachache”. Amesema Dk. Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa baadhi ya kodi zinazokusanywa na mamlaka hiyo ni kero, na kufafanua kuwa TRA wameagizwa kukusanya kodi kila sehemu lakini sio kwa njia ya kudhulumu wananchi. Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa wamachinga kutumia vizuri fursa ya kufanya biashara kila sehemu na kuwataka kutokwepa kodi.
“Serikali isiyokusanya mapato ni serikali mfilisi, niwaombe sana waficgueni watu wenye tabia hiyo ili wasiwaharibie na muwe mnatoa elimu na sio kupeleka polisi kuwakamata wananchi wanaposhindwa kukusanya kodi”. Amesema Rais Magufuli.