Home FEDHA Umaskini, ukosefu wa maendeleo miongoni mwa changamoto Afrika

Umaskini, ukosefu wa maendeleo miongoni mwa changamoto Afrika

0 comment 185 views

Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo umasikini, ukosefu wa maendeleo, ajira, amani na usalama na kutokuwa na sauti moja katika majukwaa ya kimataifa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa Shaib amesema hayo wakati akifungua Semina ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo.

Akifungua semina hiyo Jijini Dar es Salaam, Balozi Said amesema nchi za Afrika lazima ziendelee kupambana ili kuhakikisha Afrika inayotakiwa inafikiwa na kuweza kutatua changamoto zinazoikabili Afrika.

Ameeleza kuwa Tanzania imejidhatiti kutekeleza Ajenda 2063 na Ajenda 2030 kwakuwa zimewekwa katika mipango ya maendeleo ya Taifa na kutekelezwa kupitia mipango hiyo.

Amesema Tanzania imepiga hatua katika kutekeleza malengo ya Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 na hivyo kuendelea kuimarika kwa kiwango cha ukuaji ambacho amesema kuwa kinatarajiwa kuendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 5 kwa mwaka 2024 na kuendelea.

“Kiwango hicho cha ukuaji kimechochewa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu na uwekezaji inayotekelezwa na Serikali katika sekta mbalimbali,” amesema.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Barabara, Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere pamoja na urekebishaji wa miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege nchini.

Amesema Tanzania imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kutokomeza njaa nchini na kuongeza kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa kuimarisha upatikanaji na usawa katika Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi (TVET) na elimu ya juu.

“Tanzania pia imefanikiwa kupunguza viwango vya vifo vya mama na watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huku ikiendelea kufurahia amani na utulivu kwa kuboresha demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria,” ameeleza.

Amebainisha kuwa “mbali na mafanikio niliyoyaeleza, bado nchi wanachama zinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063”.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter