Ni dhahiri kuwa kila mtu hutamani kupata mafanikio ya haraka ili aweze kufurahia maisha, lakini jambo hili sio rahisi na inahitaji watu kujituma ili kuweza kufikia malengo. Kupanda na kushuka kwa thamani ya fedha hutegemeana na thamani ya vitu. Kadri watu wanavyotamani kitu fulani, na thamani yake hupanda jambo ambalo kwa namna moja au nyingine thamani ya fedha.
Kuna mifumo mbalimbali ya ununuzi na ulipaji kutokana na thamani kwa mfano dhahabu na fedha. Kadri muda unavyokwenda, mifumo pia inabadilika. Watu wanatumia zaidi mifumo kama M-Pesa, Halopesa, Airtel Money na Tigopesa kufanya manunuzi na malipo na siku za hivi karibuni, wameanza kufurahia mfumo wa cryptocurrency.
Cryptocurrency ni sarafu za kidijiti ambazo huwezi kuzishika lakini unaweza kufanya mabadilishano kwa kiwango baina ya mtu na mtu, au kufanya malipo ya moja kwa moja kati ya watu. Kupitia mfumo huu mtumiaji anaweza kupokea na kutuma fedha bure duniani kote, ni mfumo wa haraka na muamala wake hufanyika kwa urahisi kama ambavyo unatuma na kupokea barua pepe. Inaelezwa kuwa kila siku sarafu mpya zinaendelea kuvumbuliwa, na hadi kufika Februari 2018, kulikuwa na sarafu zaidi ya 1400. Baadhi ya sarafu kubwa za kidigitali ni Bitcoin, Ethereum, Ripple, Bitcoin Cash, Cardano, Litecoin, Onyxcoin na nyingine nyingi.
Licha ya cryptocurrencies kuwepo tangu miaka ya 1980, umaarufu wake umekuwa mkubwa miaka ya hivi karibuni baada watu wengi kutaka kujihusisha zaidi na Bitcoin ambayo ilianzishwa mwaka 2009 na Satoshi Nakamoto lakini ikajipatia umaarufu zaidi mwaka 2017 baada ya thamani yake kupanda na kufikia Dola za Mraekani 2,000. Baada ya mfumuko huo, wengi wamechukua fursa ya kuwekeza katika cryptocurrency na leo hii, wengi wamepata mafanikio.
Kwa upande wa Tanzania, watu wengi wameanza kujikita na cryptocurrency hivi sasa, Hali ambayo imeipelekea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kueleza kuwa inafanya utafiti ili kujua athari zinazotokana na cryptocurrency katika uchumi wa nchi ili kuweza kuamua kama zabuni (Brokers) wajisajili au la.
“Tafadhali ifahamike kuwa Benki Kuu ya Tanzania inafanya utafiti ili kutathmini kiwango cha cryptocurrency na Biashara ya Forex na athari zake kwa uchumi wa Tanzania. Matokeo ya utafiti huu yataamua ikiwa kuna haja yoyote ya kusajili wazabuni wa biashara hii nchini”. Imesoma barua hiyo iliyotolewa tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Licha ya watu mbalimbali kuendelea kuanzisha kampuni ndogo, moja ya kampuni ambayo imekuwa ikijihusisha zaidi na masuala ya cryptocurrency kwa muda mrefu ni CITL International iliyopo jijini Dar es salaam
Baada ya kujua hayo, vifuatavyo ni vitu kadhaa ambavyo kila mtu anatakiwa kuzingatia:
Fanya utafiti
Ni muhimu kujua mambo muhimu ikiwa ni pamoja na hatari iliyopo katika kila uwekezaji huu. Bila kuelewa vitu vya msingi, unaweza kupata hasara na kupoteza fedha zako hivyo fahamu faida na hasara za kuwekeza katika cryptocurrency, kisha elewa mambo ya kufanya na kuepuka katika uwekezaji huu. Kabla ya kitu chochote fanya utafiti bila kuchoka ili kujua mambo mbalimbali. Hata baada ya kuamua kujihusisha na cryptocurrency, hakikisha unaendelea kufanya utafiti zaidi ili kujifunza mambo mengi zaidi kwani kadri muda unavyokwenda na mabadiliko nayo pia yanatokea hivyo ni muhimu kuwa mfuatiliaji.
Fuatilia fedha zako
Jambo la msingi ni kuepuka kuwekeza fedha ambazo una mahitaji nazo, kwani mambo yasipoenda sawa itaathiri maisha yako kwa ujumla. Ikiwa utawekeza katika cryptocurencies, hakikisha unawekeza fedha za ziada, na hata baada ya kuwekeza hakikisha unafuatilia fedha hizo kwani kuna changamoto ya wizi katika mitandao. Mfano mzuri wa hili upo katika mfumo wa Bitcoin ambapo watu wamekuwa wakitengeneza akaunti za uongo na kujifanya zabuni. Pia kuwa makini wakati unaingiza nywila (password) yako na hakikisha ni imara na wakati unavyohamisha fedha kutoka katika akaunti moja kwenda nyingine.
Ukuaji wa teknolojia umepelekea mifumo mbalimbali kuvumbuliwa na kuboreshwa ili kurahisisha zaidi huduma za kifedha. Kupitia crypotocurrency watu wengi hususani vijana wanaendelea kunufaika na kutengeneza fedha kirahisi kupitia mtandao.