Home VIWANDA Mwijage: Viwanda vidogo visibezwe

Mwijage: Viwanda vidogo visibezwe

0 comment 149 views

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema mchango wa viwanda vidogo na vile vya kati katika uchumi, maendeleo na ustawi wa nchi yoyote ni mkubwa kutokana na kwamba, vinatoa ajira kwa idadi kubwa ya wananchi ikilinganishwa na viwanda vikubwa hivyo havistahili kubezwa kwa namna yoyote. Mwijage amesema hayo alipokuwa akihitimisha maonyesho ya viwanda vidogo kitaifa yaliyofanyika kitaifa kwa mara ya kwanza mkoani Simiyu na kuongeza kuwa, viwanda vidogo ni muhimu katika uchumi wa nchi na pia hutumika kama shule na vinaweza kumilikiwa kirahisi. Waziri Mwijage amesisitiza kuwa serikali inalenga kujenga uchumi jumuishi ambao ni rahisi kufikiwa kupitia uchumi wa viwanda.

“Najua kuna watu wanapenda kubeza lakini napenda niwaeleze nafasi ya viwanda na biashara ndogo katika uchumi, maendeleo na ustawi ya nchi yoyote, Sisi Tanzania tangu uhuru mpaka leo tuna viwanda 54,000, lakini asilimia 99 ni viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati; sisi siyo kilema kwenye viwanda nchi zote zipo hivyo, viwanda vyenye tija  na vinavyoajiri watu wengi ni viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati”. Amefafanua Mwijage.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO), Prof. Sylvester Mpanduji amesema ili watanzania waweze kushiriki ujenzi wa uchumi wa viwanda, wanatakiwa kuanza na viwanda vidogo ambavyo shirika hilo litakahakikisha vinakuwa endelevu. Aidha, Prof. Mpanduji amesema maonyesho hayo yamesaidia kuwaleta wajasiriamali pamoja na kubadilishana uzoefu katika teknolojia, usindikaji na masuala mengine yanayohusu uzalishaji kupitia viwanda vidogo na vya kati.

Maonyesho ya viwanda vidogo yamefanyika kitaifa kwa mara ya kwanza, chini ya kauli mbiu “PAMOJA TUJENGE VIWANDA KUFIKIA UCHUMI WA KATI” yameshirikisha wajasiriamali takribani 515 kutoka mikoa 23 pamoja na nchi jirani za Burundi na Uganda huku mabalozi kutoka nchini Nigeria na Angola nao wakishiriki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter