Na Mwandishi wetu
Kamishina na Mtendaji mkuu wa kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Onesmo Makambe amesema Wizara ya Fedha imetayarisha kanuni za taarifa za usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu, ambazo zitawezesha nchi kufahamu takwimu kamili za usafirishaji wa fedha.
Akiwa katika ufunguzi wa maandalizi wa kanuni hizo Makambe ameongeza kuwa kupitia takwimu zitakazokusanywa, vitendo vya uhalifu na utoroshaji wa mitaji vitapungua na kumalizika kabisa. Na kwa mujibu wa kanuni hizo watakaobainika kutoa taarifa za uongo au kuacha kutoa taarifa kabisa wataadhibiwa kisheria.
Wasafiri wote watakaoingia na kutoka nchini wanapaswa kutoa taarifa ya fedha wanazosafirisha iwapo zitazifikia dola za kimarekani Sh 10,000 au zaidi. Hali hii imetokana na benki zilizopo mipakani kuongeza umakini na hivyo kupelekea wahalifu kuogopa kutumia huduma hiyo pindi wawapo safarini.
Kamishina huyo pia amewasihi wadau kutoka taasisi mbalimbali watakaoshiriki zoezi hili kuwa waaminifu na waadilifu ili kuepusha wasio na nia njema kuhatarisha usalama wa nchi yetu.
Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje, Mamlaka ya Mapato na vikosi vya ulinzi na usalama ni baadhi ya taasisi zitakazoshiriki kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa.