Na Mwandishi wetu
Baada ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. 100 milioni, Mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga ametoa agizo la kukamatwa kwa maofisa ushirika na viongozi wa vyama vya ushirika ambao wamepelekea serikali kupata hasara hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa tamko hilo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika ambalo lilihusisha halimashauri sita za mkoani humo kwa lengo la kuimarisha nguvu ya kukuza uchumi kwa vijana. Ameongeza kuwa vyama vya ushirika 139 vimekufa mkoani Geita kutokana na usimamizi mbovu wa viongozi hivyo kuipa serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde amesema kinachopelekea vyama vya ushirika vya kilimo, ufugaji, uvuvi, akiba, mikopo na uchimbaji wa madini kuporomoka ni utendaji mbovu wa viongozi waliochaguliwa. Ametaka vyama hivyo kuchagua viongozi waadilifu ambao watasimamia miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wote.