Ofisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka amesema walengwa wakuu wa msamaha maalum wa riba pamoja na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 ni kampuni, taasisi na watu binafsi wanaowasilisha ritani za kodi, lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zinazotokana na ritani hizo.
“Walengwa wengine ni wale wote ambao hawajawasilisha ritani za kodi, hawajasajiliwa na kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) au namba ya usajili wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na wale waliowasilisha pingamizi au rufaa za kodi ambazo bado zinashughulikiwa katika ofisi za TRA, bodi ya rufaa na mahakama ya rufani za kodi”. Amefafanua Ofisa huyo.
Mbali na hayo, Mahendeka amewataja ambao hawahusiki na msamaha huo kuwa ni wale ambao wangestahili kupata msamaha lakini wameshalipa madeni yao pamoja na wale ambao masuala yao ya kikodi yapo katika hatua ya ukaguzi au uchunguzi.
“Wengine ambao hawahusiki na msamaha huu ni taasisi, kampuni na watu binafsi ambao wana madeni ya nyuma ya kodi yanayotokana na adhabu zilizoamuliwa tayari au adhabu za makosa yatokanayo na uzembe wa kukusudia uliobainika kisheria pamoja na wenye riba au faini zilizotokana na kutoa au kutumia risiti za kielektroniki za kughushi”. Ameeleza Mahendeka.