Home FEDHA Zoezi la kuondoa noti za zamani kuanza Januari 06, 2025

Zoezi la kuondoa noti za zamani kuanza Januari 06, 2025

0 comment 245 views

Zoezi la kuondoa noti za zamani kwenye mzunguko wa fedha linatarajiwa kuanza January 06, 2025 hadi Aprili 05, mwakani.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeeleza hayo wakati wa kutoa elimu kwa waandishi wa habari nchini kufafanua kuhusu taarifa iliyotolewa hivi karibuni inayohusu zoezi la kuondoa noti hizo kwenye mzunguko.

BoT imeeleza kuwa zoezi hilo litafanyika kupitia ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.

Noti hizi ni za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003, na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la Oktoba 11, 2024.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu, Ilulu S. Ilulu, amesema Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inaipa mamlaka BoT kuchapisha, kutangaza na kusambaza noti nchini.

“Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, sura ya 197, kifungu cha 26, kimeipa Benki Kuu mamlaka ya kuchapisha noti na kuzisambaza nchini Tanzania.

Kifungu cha 27 (2), kimeipa mamlaka BoT kuzitangaza noti ambazo itakuwa imezichapisha ikiwemo kutoa tangazo katika Gazeti la Serikali kabla ya noti hizo kuingizwa kwenye mzunguko kwa ajili ya matumizi,” amesema Ilulu.

Ameongeza kuwa Sheria hiyo inailekeza BoT kutoa muda wa kurejesha noti zilizoainishwa kwa ajili ya ukusanyaji wa noti hizo pamoja na kuziondolea uhalali wa kutumika.

Aidha, amesisitiza kuwa zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani siyo geni nchini na lilifanyika mara ya kwanza mwaka 1977.

“Tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu mwaka 1966, mazoezi ya kuondoa noti kwenye mzunguko yamefanyika mwaka 1977, 1979, 1980 na 1995. Kwa hiyo, kama tulivyoeleza, hii ni kazi ya kawaida ya Benki Kuu hapa nchini na ulimwenguni kote.”

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter