Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Kazi ya ndoto yako au Kazi ya kuingiza kipato tu?

Kazi ya ndoto yako au Kazi ya kuingiza kipato tu?

0 comment 99 views

Ajira imeendelea kuwa changamoto kubwa wa watu wengi. Kuna ambao wamebahatika na kupata kazi ambazo huenda zinawalipa vizuri tu lakini bado hawazifurahii. Hali hii ipo kote duniani sio hapa kwetu pekee. Kundi kubwa la waajiriwa wanafanya kazi ambazo hawazifurahishi sababu tu zinawawezesha kumudu familia na maisha kwa ujumla. Wachache sana hutafuta na kupata kazi ambazo wanazipenda na kuzifurahia. Soko la ajira limechangia kwa kiasi kikubwa katika tatizo hili kutokana na ugumu wake. Wengi huishia katika kazi ambazo wanazifanya tu ili walipwe na waweze kukabiliana na ugumu wa maisha.

Kama kundi kubwa la waajiriwa wapo katika nafasi zao ili tu kujikumu huduma wanazotoa zinaathirika kwa namna yoyote ile? Wanakuwa na moyo wa kutoa huduma kwa haki na usawa? Wanajali kuhusu wale wanaowahudumia? Wanazingatia haki za msingi za wataka huduma wao? Au yote haya sio muhimu kwa sababu tu mwisho wa siku wanapata kipato chao?

Lakini ni muhimu kujiuliza mzizi haswa wa tatizo hili ni nini? Ugumu wa maisha umepelekea watu kukubali kufanya kazi yoyote? Kwanini ni asilimia ndogo tu ya watanzania wanafurahia ajira zao na kutekeleza majukumu yao kwa moyo mmoja?

Suala hili linapaswa kuangaliwa na kupewa uzito kwani kuna baadhi ya sekta kama vile elimu, afya na fedha zinawagusa wananchi moja kwa moja hivyo huduma isiyoridhisha inaweza kumuathiri mtu kwa kiasi kikubwa. Ni kweli kwamba ili kutimiza wajibu wako sehemu ya kazi ni lazima uwe na ujuzi, elimu na uzoefu unaotakiwa lakini kuna sababu ya kutoa elimu kwa umma hasa kwa jamii kama vile wanafunzi ili kuwafundisha umuhimu wa kupenda kile unachofanya. Kufanya hivi kutawatayarisha mapema kabla hawajaingia rasmi katika soko la ajira.

Ni kweli kwamba tunahitaji kipato kizuri ili kuweza kuendesha maisha yetu na kumudu mahitaji mbalimbali ya familia. Hakuna anaeweza kubishana na hilo. Lakini ongezeko kubwa la watu kufanya shughuli yoyote tu ambayo itawasaidia kujikimu halipaswi kufumbiwa macho. Kuna ugumu katika kupata kazi unayopendelea au kiwango cha mshahara ni kidogo? Fikiria, kama wahitimu mia moja (100) wa tasnia fulani wakiachana na kazi ambayo wameisomea na kutafuta kazi nyingine ambayo inalipa vizuri taifa inapoteza wataalamu wangapi kila mwaka?

Mwisho wa yote kipato unachopata ndicho kinaendesha maisha na sio vinginevyo. Lakini ni vizuri kuwepo na uwiano baina ya mambo haya mawili ili kuhakikisha kuwa japokuwa unaingiza kipato kizuri kinachofanikisha malengo yako mengine ya maisha, bado una heshima na nidhamu na kazi unayofanya na unatoa huduma stahiki kwa walengwa au jamii kwa ujumla.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter