Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Augosti 17, 2021 amezungumza na kujitambulisha rasmi katika mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Jijini Lilongwe nchini Malawi.
Katika mkutano huo, Rais Samia amegusia mambo mbalimbali ikiwemo demokrasia, uchumi na ugonjwa wa UVIKO-19.
Rais Samia amesema Jumuiya hiyo imekuwa na mafanikio mengi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980.
“Tumeshuhudia kuongeza kwa demokrasia ikiwemo utaratibu wa kubadilishana uongozi,” amesema Rais Samia akitolea mfano nchi ya Zambia ambayo ilikuwa kwenye uchaguzi hivi karibuni.
Kwa upande wa uchumi amesema takwimu zinaonyesha kuimarika kwa uchumi na ukuaji wa biashara.
“Tusiridhike kwani bado tuna changamoto za uchumi, ajira, usalama, maswala ya ugaidi magonjwa, uhalifu wa kimataifa na uhaba wa stadi za kazi kwa wananchi.” Amesema Rais Samia.
Akizungumza kuhusu suala la ugonjwa wa UVIKO-19, Rais Samia amesema mahitaji ya chanjo bado ni makubwa.
Amesema lengo la serikali yake ni kuhakikisha wananchi wote wanachanjwa ili kupata kinga ya ugonjwa huo na kuziomba nchi za SADC kushawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia vibali na teknolojia zao zitumike ili kuruhusu chanjo kuzalishwa katika nchi mbalimbali kukidhi mahitaji yaliyopo.
Katika hotuba yake Rais Samia amesema Malawi ni Taifa la kwanza katika nchi za SADC kuongozwa na Rais mwanamke, hivyo kujitambulisha kwake katika mkutano huo kutaongeza msukumo kwa wanawake wengi zaidi kujiamini na kuhamasika kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.
Amewasihi viongozi wa SADC kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi katika nchi zao.
Amempongeza Rais wa Malawi Dkt Lazarus Chakwera kwa kuchaguliwa mwenyekiti mpya wa SADC na pia amempongeza Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi kwa kuongoza Jumuiya hiyo kwa mwaka uliopita.
Aidha, ameahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu na mwadilifu katika Jumuiya hiyo.