Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Mfumo wa Taifa wa Takwimu kusaidia maendeleo

Mfumo wa Taifa wa Takwimu kusaidia maendeleo

0 comment 158 views

Mfumo wa Kitaifa wa Takwimu utasaidia nchi kuweka mipango yake ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, wa mwaka 2020 – 2025 na maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa 2025 – 2030.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amesema mfumo huo unafanya kazi kwa ufanisi, gharama nafuu na wenye uwezo wa kutoa takwimu bora na za uhakika.

Dkt. Mwamba amesema hayo wakati akifungua kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ya Pamoja ya Awamu ya Pili ya Mpango Kabambe wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu nchini, (Tanzania Statistical Master Plan II), Jijini Dar es Salaam.

Mpango Kabambe wa Pili wa Takwimu nchini unafadhiliwa kwa sehemu na mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Kimarekani milioni 82, chini ya Mpango wa Takwimu wa Kanda ya Afrika Mashariki, unaotekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya na Rwanda.

Amesema katika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya takwimu na changamoto za upatikanaji wake, Serikali imekuwa ikichukua hatua za makusudi za kuimarisha uzalishaji wa takwimu nchini ukiwemo Mpango Kabambe wa Pili wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2022/23 hadi 2026/27.

“Mpango huu unakusudiwa kudumisha na kuendeleza mafanikio ya Mpango Kabambe wa Kwanza wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu kwenye vipengele vikuu vitatu.

Vipengele hivyo ni Uratibu, Ubora na Usambazaji wa Takwimu, Uzalishaji wa Takwimu na Miundo ya kitaasisi na Miundombinu,” amesema Dkt. Mwamba.

Amebainisha kuwa Serikali inatambua mchango na ushirikiano mkubwa kutoka kwa washirika wa maendeleo, sekta binafsi, wanataaluma, Asasi za Kiraia na wadau wengine katika kuimarisha Mfumo wa Kitaifa wa Takwimu kupitia misaada yao ya kifedha na kiufundi na kwamba bado vitu hivyo vinahitajika katika safari ya kuimarisha takwimu.

“Nitumie fursa hii kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Mkutano huu na kwa niaba ya Serikali kutoa shukrani zangu za dhati kwa Benki ya Dunia na washirika wetu wote wa Maendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter