Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tanzania, Uganda zatia saini mkataba wa ujenzi bomba la gesi

Tanzania, Uganda zatia saini mkataba wa ujenzi bomba la gesi

0 comment 201 views

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda zimetia saini mkataba utakaowezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda.

Mkataba huo umesainiwa Novemba 09, 2023 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania Dkt. Doto Biteko pamoja na Ruth Nankabirwa, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Jamhuri ya Uganda.

Dkt. Doto Biteko amesema kusainiwa kwa mkataba huo kumetokana na makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding – MoU) kati ya nchi hizi mbili yaliyosainiwa mwezi Agosti, mwaka 2018 kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda kutokana na Tanzania kugundua kiasi kikubwa cha gesi katika kina kirefu cha bahari na nchi kavu.

“Nchi hizi mbili zimekubaliana kufanya kazi ya upembuzi yakinifu kwa pamoja kuwezesha tathmini ya mradi na kutoa muongozo wa uwezekano wa mradi ikiwemo muundo wa mradi, mahitaji ya gesi, ukubwa wa bomba na taarifa nyingine muhimu zinazohusu mradi huo kwa ajili ya kufanya maamuzi,” amesema Dkt. Biteko

Amebainisha kuwa nishati ni ufunguo wa maendeleo kwa nchi yoyote ile duniani na umoja ni nguvu hivyo ametoa wito kwa nchi hizi mbili kutumia fursa ya kutekeleza mradi huu ambao utaunganisha nchi hizi mbili katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa, licha ya Tanzania kugundua kiasi kikubwa cha gesi asilia takiriban futi za ujazo trilioni 57.54, mahitaji ya rasilimali hiyo yanakua kwa kasi ndani na nje ya nchi.

“Hii inapelekea Serikali kuweka nguvu zaidi katika utafutaji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Eyasi Wembere, Mnazi Bay Kaskazini, Songosongo Magharibi, Ziwa Tanganyika na katika kina kirefu cha maji baharini,” amesema.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter