Jambo moja la msingi katika ufugaji wa kuku ni mabanda ya kufugia na kutokana na ubora wake, mfugaji anaweza kupata mafanikio au hasara kwani kuku hukua na hutaga zaidi katika mazingira mazuri na salama.
Siku hizi kuna mabanda ya kisasa yaliyo katika mfumo wa betri ambayo yanamrahisishia mfugaji kufuga katika hali ya usafi na salama. Wafugaji wengi ambao wanatumia mabanda hayo wamekuwa wakifurahia matokeo.
Bei zake hutegemea aina ya banda na kiasi cha kuku waliopo lakini kwa makadirio mabanda mengi ya kuku ya kisasa ya mfumo wa betri huuzwa kati ya Sh. 450,000 (kwa ajili ya vifaranga), uwezo wake ukiwa vifaranga 400, na kwa kuku wakubwa (layers) huuzwa kwa Sh. 750,000 na uwezo wake ni kuku 96 katika banda moja.
Hizi ni faida nne za kutumia mabanda ya kisasa katika ufugaji wa kuku hususani wa mayai:
Huokoa nafasi
Kwa wafugaji wa kuku ambao wana changamoto ya nafasi kwa ajili ya kufugia wanaweza kusuluhisha changamoto hiyo kwa kutumia mfumo wa kisasa wa mabanda ya kufugia, kwani katika mabanda hayo ya kisasa huwa kunakuwa na nafasi ambayo kuku wanaweza kufugwa katika mpangilio mzuri zaidi.
Kwa mfano kuna mabanda ambayo yanaweza kufuga kuku 96, kuna mabanda ambayo hukaa kama gorofa ambayo huruhusu ufugaji wa kuku 128 hadi 300 hivyo mkulima anaweza kununua banda ambalo linakidhi kiasi cha kuku anaotaka kufuga bila kuwaza kuhusu nafasi.
Ubora
Kupitia mabanda ya kisasa mfugaji hupata urahisi wa kulisha vizuri kuku na kuwatunza kwa umakini zaidi jambo ambalo hupelekea kuku kuwa na afya njema na kutaga mayai bora yaliyo katika hali ya usafi ambayo mwisho wa siku mkulima huyapata katika mfumo ambao tayari umetengenezwa katika mabanda hayo hivyo kuepuka upotevu wa muda kwa kuanza kusafisha, jambo ambalo linaweza kusababisha mayai yachelewe kuwafikia wateja kwa wakati.
Kupitia mabanda haya ufugaji wa kuku wa mayai umerahisishwa na kumuwezesha mfugaji kapata bidhaa bora.
Gharama
Mabanda ya kisasa yaliyo katika mfumo wa betri yamerahisisha kazi kwa asilimia kubwa hivyo hakuna haja ya kuajiri watu wengi kwa ajili ya kuangalia kuku.
Kila kitu kimeshapangwa katika mfumo huo, ikiwa ni pamoja na mpangilio wa kuku wenyewe, sehemu maalum ya kulisha na kuwawekea maji, sehemu ya mayai kupita na sehemu ya mfugaji kuchukua mayai hayo.
Kazi iliyopo ni kuwamiminia chakula na maji kupitia maeneo yaliyotengwa na kuhakikisha mayai na uchafu yanatolewa kila baada ya muda ili kuku waendelee kutaga katika mazingira safi na salama.
Hupunguza magonjwa
Kutokana na kila kuku kuwa na sehemu yake si rahisi kuambukizana magonjwa. Pia mfumo maalum wa kutolea kinyesi unafanya iwe ngumu kwa kuku kufikia kinyesi chao na kupata maambukizi mbalimbali.
Vilevile ni rahisi zaidi kutambua na kuchukua hatua kwa kuku wenye magonjwa kabla hawajasambaza kwa kuku wengine.
Aidha, ni muhimu kwa wafugaji kupewa elimu zaidi kuhusu teknolojia za kisasa zinazohusiana na ufugaji ili kuweza kunufaika na ufugaji wao bila kutumia nguvu nyingi.
Watanzania wengi wameendelea kuwekeza katika sekta hii ya ufugaji hivyo ni wakati muafaka kwa serikali na wadau mbalimbali kuwaunga mkono kwa kuwapa elimu sahihi.