Uharibifu wa miundombinu ya reli umesababisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kusitisha huduma za safari za treni kwa muda kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na TRC Januari 17, 2024 imetaja maeneo yaliyoharibiwa na mvua kuwa ni Mazimbu, Kilosa na Munisagara mkoani Morogoro, Godegode na Gulwe (Dodoma), Ruvu Junction, Wami, Mvave mkoani Pwani pamoja na eneo la Mkalamo mkoani Tanga.
Safari zilizositishwa ni kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Katavi, Kigoma, Shinyanga na Mwanza pamoja na mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
“Wahandisi wa TRC wanaendelea na matengenezo katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa huduma za usafiri wa treni zinatarajiwa kuanza Januari 23, 2024 katika reli ya kati na kwa mikoa ya Kaskazini (Kilimanjaro, Tanga na Arusha inatarajiwa kuanza Januari 29, 2024 baada ya ujenzi kukamilika.
TRC imewasihi wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi cha matengenezo huku ikiwaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.