Kila mtu anatamani kuacha kazi na kujiajiri Sababu za kutamani mabadiliko hayo hutofautiana kwa kila mtu. Mara nyingi kujua mambo ya msingi kuhusu jambo unalotaka kufanya hurahisisha utekelezaji wa jambo hilo, hali hiyo pia ipo katika ujasiriamali. Pamoja na hayo, kuna baadhi ya mambo ambayo watu wengi hupuuza pale wanapoanza safari yao na hii imepelekea kushindwa na kupoteza fedha. Kwa wengine, imepelekea kupitia vikwazo vingi hata kama hawakukata tamaa.
Ikiwa unafikiria kuwa mjasiriamali, ni muhimu kuzingatia yafuatayo:
Usitengeneze bidhaa mpya, suluhisha tatizo/shida
42% ya bidhaa zinazozinduliwa kila siku hushindwa kwa sababu hakuna uhitaji wa bidhaa hizo. Hivyo badala ya kutumia muda mwingi kutengeneza bidhaa mpya jaribu kutafuta bidhaa zinazoweza kusuluhisha matatizo au shida za watu katika maeneo husika.
Sahau mafanikio ya haraka
Hata kampuni ambazo zimekua kwa kasi hazikupata mafanikio yake ndani ya muda mfupi, inawezekana zilijijenga na kujipanga kwa muda wa miaka mrefu kabla ya kupata mafanikio. Baadhi ya kampuni huchukua hata miaka 10 au zaidi kufanikisha malengo. Ikiwa unataka kutajirika kupitia biashara yako, unapaswa kuwa mvumilivu.
Zingatia nguvu na sio udhaifu wako
Mafanikio yatatokana na nguvu zako kwa hivyo hakikisha muda wako mwingi unatumia katika eneo hilo. Sisi sote tuna udhaifu, ili kukabiliana na udhaifu huo inashauriwa kuajiri watu ambao wana nguvu katika eneo hilo ili kuongeza nguvu ya ufanisi. Siku zote kuzingatia udhaifu kunaweza kusababisha ushindwe kufanya mambo ambayo una uzoefu na nguvu nayo.
Kuwa na timu inayofaa
Huwezi kufanya kila kitu wewe mwenyewe, lazima utahitaji msaada. Jambo la msingi ni kupata msaada sahihi. 29% ya kampuni zinazoanza hushindwa kwa sababu walikuwa na timu isiyofaa. Tumia muda kuangalia timu unayoihitaji kisha ajiri watu wenye ujuzi unaotakiwa.
Ikiwa utashindwa, kufeli ni sehemu ya mchakato hivyo unatakiwa kujipanga. Njia rahisi ni kukubaliana na mabadiliko na kujaribu tena. Kushindwa taratibu huku ukitegemea kuwa siku moja mabadiliko yatatokea ni kujidanganya na kunaweza kusababisha upoteze biashara yako.
Jua pendekezo lako la thamani
Ikiwa hujui thamani ya kila unachouza itakuwa ni shida hata kwa wateja, kwa sababu hawataelewa ni nini hasa kinatofautisha biashara yako na ya wengine. Kurahisisha na kuweka wazi pendekezo la bidhaa yako kutarahisisha watu kuamua kama wanahitaji huduma yako au la.
Jua wateja wako
Siku zote urahisi wa kuelezea unaelekeza bidhaa zako kwa watu wa aina gani, rika gani kutarahisisha mafanikio katika biashara au kampuni. Wateja ndio msingi wa mafanikio hivyo hakikisha unajua bidhaa zako unalenga kuwauzia watu wa aina gani.
Sio kila mteja anakufaa
Ni muhimu kujua “si kila mteja ni mteja sahihi” hasa kama ana hatarisha mafanikio ya kampuni yako. Kama ambavyo kuna bidhaa mbaya na kampuni, pia kuna wateja wabaya na unatakiwa kuachana nao na kujikita katika kutafuta wateja sahihi.
Jifunze kutokana na makosa
Makosa ni fursa nzuri ya kujifunza lakini haimaanisha unatakiwa kufanya makosa kila wakati. 80% ya kampuni zinazoanza hushindwa. Jifunze kwanini kampuni hizo zilifeli ili kuepuka mitego hiyo. Hii itakusaidia kuokoa muda na fedha nyingi.
Hakuna biashara, hakuna mauzo
Mauzo ni kama pumzi, bila mauzo biashara lazima ishindikane. Biashara haiwezi kujiendeleza kwa sababu ya wazo, bidhaa na huduma pekee, Ni muhimu kujitangaza, kuhamasisha wateja ili waweze kununua.