Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Mbegu za maboga ni fursa mpya mjini

Mbegu za maboga ni fursa mpya mjini

0 comment 242 views

Siku za hivi karibuni imeshuhudiwa biashara mpya ikiibuka mjini huku watu waliopo vijijini wakiwa bado hawajaigundua fursa hii ya kiuchumi hasa katika shughuli za kilimo.

Nikiwa maeneo ya makumbusho naamua kuingia supermarket moja mpya iliyojengwa hivi karibuni. Moja ya vitu vinavyonishangaza ndani ya supermarket hiyo ni kukutana na bidhaa ya mbegu za maboga.

Ni kitu ambacho sikutegemea kukutana nacho katika maeneo hayo ukizingatia supermarket ni moja ya sehemu ambayo huuzwa vitu ghali na vyenye kupendeza. Nilipojaribu kuuliza bei nikaambiwa pakiti moja inauzwa Tsh. 1000.

Kwa jamii nyingi za Tanzania biashara hii ni mpya kabisa kwa sababu walio wengi wamekuwa wakiitupa bidhaa hiyo huku wakiamini kitu cha muhimu katika zao hilo ni maboga na majani yake ambayo ni mboga.

Hii ni fursa mpya ya kiuchumi ambayo lazima itiliwe mkazo ukizingatia ukweli kwamba biashara hii imekuwa ikikua kwa kasi.

Pesatu.com imejaribu kuwauliza wakazi wa Nyanda za juu kusini ikiwa ni moja kati ya jamii zinazolima zao hili katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa ambao wengi wamekiri mbegu za Maboga zimekuwa zikiuzwa 4000 hadi 6000 kwa sado hasa maeneo ya vijijini huku wakazi wengi wa maeneo hayo wakiwa bado hawachukulii mbegu za maboga kama fursa ya kiuchumi.

Soko la Kisutu lililopo maeneo ya Posta Jijini Dar Es Salaam ni moja kati ya masoko maarufu hapa jijini kwa uuzaji wa vyakula na mazao, ikiwemo, matunda, mboga za majani na nafaka, Pesatu.com iliweka kambi mwishoni mwa wiki hii na kufanya mahojiano na Bwana Saleh Abdul mmoja kati ya wauza nafaka waliopo katika soko hilo ambaye alikiri wazi kuwa bidhaa hiyo imekuwa ikipanda bei kila siku huku nusu kilo ya Mbegu hizo ikiuzwa kwa Tsh. 4000 sawa na 8000 kwa kilo.

Hata hivyo inashauriwa kuwa mkulima wa zao hili ni ni vema akafuata ushauri wa kitaalamu hasa juu ya mbegu bora yenye kuzalisha mbegu nyingi za maboga.

Kwanini bidhaa hii imekuwa kwa kasi kiasi cha kuuzwa Supermarket?

Bidhaa hii inakua kila iitwapo leo kutokana na kazi kubwa za mbegu hizo katika mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na kuzuia ugonjwa wa kisukari,mbegu hizi zina kiasi kikubwa cha madini ya Zinc yanayosaidia kuimarisha kibofu cha mkojo,Kinga ya Saratani ambapo Imethibitika kwamba watu ambao hula mlo wenye kiasi kingi cha mbegu za maboga wamegundulika kuwa na hatari ndogo sana ya kupatwa na saratani za tumbo, matiti, mapafu na kibofu, dawa ya uvimbe ikithibitishwa na tafiti kadhaa ambazo zimeonesha kuwa mbegu za maboga zina mafuta yenye uwezo wa kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya uvimbe (inflamatory diseases) sawa na dawa aina ya Indomethacin, lakini mbegu hizi hazina madhara kama ilivyo kwa hiyo dawa.

Nini kifanyike ili kuhakikisha uzalishaji wa kutosha wa zao hili?

Wazalishai wengi wa zao hili wanapatikana maeneo ya vijijini na bado hawachukulii suala hili kama fursa ya kiuchumi, hivyo elimu ya kutosha lazima itolewe ili kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wa kutosha na upatikanaji wa uhakika wa bidhaa hii sokoni kwa kuwaelimisha wakulima wa maboga kuichukulia kama fursa mpya ya kiuchumi.

Kupanga bei moja na inayoeleweka katika soko,Ukiangalia kwa makini hakuna uwiano kati ya bei za wazalishaji na bei katika soko. Wakulima wanauza sado moja kwa Tsh 4000 hadi 6000 huku wafanyabiashara wakiuza nusu kilo kwa Tsh. 4000

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter