Watu wengi wamekuwa wakitamani kuanzisha kuanzisha biashara zao lakini namna hasa ya kuanza mchakato huu imekuwa changamoto. Ujasiriamali sio kitu kirahisi endapo umekosa muongozo utakaokupa muelekeo sahihi. Kama unafikiria kuanzisha biashara yako mwenyewe, hizi ni baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kukusaidia kutimiza malengo yako:
- Kama hufurahishwi na mahali ulipo hivi sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko. Kulaumu haitasaidia chochote. Usipoteze muda mwingi kutafuta ajira kwani mamia ya wahitimu nao wanafanya hivyo na wigo wa ajira ni mdogo. Fanya maamuzi sahihi kwa ajili yako na badilisha muelekeo wa maisha yako.
- Tambua biashara gani inakufaa. Kabla ya kufanya maamuzi yoyote fanya utafiti wa biashara gani hasa inakufaa. Tumia muda wa kutosha kufanya uchunguzi na jiulize je, nitaweza kuimudu biashara hii? Ni muhimu kufanya kitu ambacho tayari unakifahamu. Sio mbaya kujifunza kutoka kwa watu ambao tayari wanafanya kitu kinachokufurahisha.
- Mpango wa biashara. Watu wengi huanzisha biashara pasipo kuwa na mpango maalum. Hili ni kosa kubwa kwani kabla ya kuwekeza unapaswa kujiuliza unawekeza kwenye nini hasa? Utamuuzia nani? Lengo lako ni nini? Vipi kuhusu matarajio? Hakikisha unaandika mpango wako wa biashara ili utakafungua mradi wako, mpango huo ukuongoze kufikia malengo yako.
- Kabla ya kufungua biashara ni lazima utambue soko lako. Jambo hili ni muhimu sana. Kabla ya kufungua duka ni lazima kujua nani hasa ni mteja wako. Hupaswi kukurupuka kwani ushindani sokoni ni mkubwa hivyo unapaswa kuwalenga watu fulani. Fanya utafiti na tambua soko lako kabla ya kuwekeza kwenye biashara unayofikiria.
- Jipange kifedha. Kama mjasiriamali hii ni muhimu ili kuhakikisha kuwa matumizi yako binafsi hayaingiliani na matumizi ya biashara. Kuwa makini na matumizi yako ya fedha kwani biashara yako inaweza kuathirika moja kwa moja kama ukiendekeza matumizi makubwa kuliko kipato unachoingiza. Wataalamu wanashauri kuwa na akaunti mbili za matumizi, moja kwa ajili ya biashara na nyingine ya matumizi binafsi ili kurahisisha mchakato mzima.
- Ili kuwa na soko la uhakika ni lazima kujitangaza na kuwafahamisha watu kuwa unatoa huduma fulani. Mitandao ya kijamii imekuwa ikichangia mafanikio ya biashara kwa kiasi kikubwa kutokana na urahisi wake wa kuwafikia mamia ya watu kwa haraka. Hakikisha biashara au huduma yako inafahamika.
- Usishindane na waliofanikiwa. Usitumie muda mwingi kutaka kuwapiku wale ambao umewakuta kwenye soko. Jifunze kutoka kwao kwani wana ujuzi zaidi. Waheshimu na jenga mahusiano mazuri. Boresha biashara yako ili kuwavutia wateja.
Hizo ni baadhi tu ya mbinu ambazo unaweza kufuata ili kufanikiwa katika ujasiriamali. Ni muhimu kuuliza maswali pale unapokwama na usisite kuomba ushauri kwa wajasiriamali wengine. Sekta hii imekuwa mkombozi wa vijana wengi na imesaidia sana kupunguza tatizo la ajira.