Bila shaka umewahi kusikia stori kuhusu watu ambao wamefanikiwa kuendesha maisha yao kwa kupitia fedha zinazotokana na mtandao wa YouTube pekee. Siku hizi, vijana wengi wamekuwa wakigeukia ujasiriamali katika teknolojia kutokana na idadi kubwa ya watuamiaji wa mitandao. Kupitia YouTube, waandaaji wa video wanaweza kuingiza fedha kwa kupitia njia mbalimbali na hivyo kuendesha maisha yao vizuri. Ni kweli kuwa unpokuwa na idadi kubwa ya wafuatiliaji, ni rahisi zaidi kutumia fursa hiyo kutengeneza fedha zaidi lakini hii haimaanishi kuwa watu walio na idadi ndogo ya wafuatiliaji hawapati chochote. Ukiwekeza muda, nguvu na jitihada za kutosha, YouTube ni sehemu ambayo inaweza kukupa utajiri mkubwa.
Kama ilivyo sehemu nyingine, YouTube nayo ina masharti na vigezo vya kuzingatia kama ifuatavyo:
- Ni lazima chaneli iwe imetumika kwa angalau miezi mitatu.
- Chaneli inatakiwa kuwa na views zisizopungua 10,000.
- Mmiliki anatakiwa kuhakiki chaneli kwa kutumia simu ya mkononi.
- Chaneli inapaswa kuwa na wafuatiliaji (Subscribers) angalau mia moja.
- Ni lazima kuwa raia wa nchi zinazokubaliwa na YouTube kupokea malipo yako.
- Ni lazima kuwa na akaunti ya Adsense.
Hizi hapa ni njia nne za kutengeneza fedha YouTube:
Google Adsense: Hii ndio njia maarufu zaidi ya kutengeneza fedha kupitia YouTube duniani kote. Adsense inamilikiwa na kampuni ya Google na kazi yake kuu ni kuwawezesha wafanyabiashara kuweka matangazo yao ya biashara katika chaneli yako. Kupitia Adsense, mmiliki wa chaneli ya Youtube hatokuwa na mahusiano ya moja kwa moja na makampuni. Badala yake, mmiliki atakuwa Adsense kama ilivyo baina ya wafanyabiashara na Adsense. Google Adsense inasimama kama dalali ambaye biashara mbalimbali hutumia ili kupata wateja.
Kuwa wakala wa biashara kubwa: Unaweza kuingiza kipato kizuri kwa kuwa mshirika au wakala wa makampuni makubwa kutoka duniani kote. Unachotakiwa kufanya ni kuweka kiunganishi (link) ndani au hata chini katika maelezo ya video yako kuelezea bidhaa husika na jinsi watu wanavyoweza kuipata. Endapo mtu atanunua bidhaa hiyo kupitia ‘link’ yako, basi utapata gawio lako. Watu wengi zaidi wanaponunua kupitia wewe ndivyo gawio lako linavyozidi kuongezeka. Baadhi ya makampuni yanayokubali uwakala ni pamoja na Amazon na eBay.
Uza bidhaa zako mwenyewe: YouTube ni mahali pazuri pa kujitangaza na kuwafikia watu kutoka sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja. Unaweza kutumia nafasi hiyo kutangaza biashara yako kwa wateja na kuingiza kipato kizuri. Jambo moja zuri kuhusu hili ni kwamba, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu hushawishika zaidi kununua kupita matangazo ya video hivyo hii ni fursa nzuri za kutambulisha biashara yako sokoni na kujitengenezea kipato.
Ushauri: Ikiwa una maarifa na unaweza kutoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali, unaweza kujiajiri kwa kuandaa video zenye ubora wa hali ya juu kushauri wafuatiliaji wako. Unapofanya hivi kwa muda mrefu na kujenga uaminifu, ni rahisi kuwashawishi watu kujiunga na huduma yako ili kupata mafunzo zaidi. Unaweza kutoza kiasi fulani cha fedha katika huduma hizo. Kama unafanya vizuri ni rahisi kwa watazamaji kulipia huduma hiyo kutokana na maarifa watakayopata.
Ikiwa unafikiria kujiajiri, teknolojia ni sekta ambayo inaendelea kukua kila siku hivyo soko lake ni la uhakika. Kama wewe ni mtaalamu katika masuala ya video basi YouTube ni kwa ajili yako. Tumia njia zilizoelezwa hapo juu kuwafikia watu wengi na kujitengenezea kipato cha uhakika. Kikubwa ambacho kinahitajika katika kazi hii ni ubora wa hali ya juu na kuwa na mada ambazo zinawagusa watu moja kwa moja.