Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) William Erio, amesema shirika hilo lina mpango wa kutumia vitambulisho vya wajasiriamali kwa ajili ya kuwasajili wanachama wapya wanaojiunga na mfuko huo kwa upande wa sekta isiyo rasmi.
Erio ameeleza kuwa mfuko huo unatumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutunza kumbukumbu za fedha hivyo kuongeza udhibiti wa ndani na usahihi wa taarifa. Pia amesema mfuko huo umeshasajili mfumo mpya wa sekta isiyo rasmi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii (SSRA).
“Tumepanga kuyafikia makundi mengine kwa kutumia vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na serikali kwa kuwasiliana na mamlaka ya serikali za mitaa na mikoa. Pia moja ya mafao tutakayotoa ni bima ya afya na tayari tumeanza mazungumzo na NHIF ili fao hilo litolewe na mfuko huo”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa licha ya kuanza kutumia rasmi mfumo mpya wa kielektroniki Mei mwaka huu kufanya usuluhishi wa kibenki, mfuko huo unaendelea kufuatilia agizo la mambo ya usuhishi wa fedha kutoka benki.
“Masuala ya usuluhishi wa kibenki yalikuwa na changamoto kutokana na zoezi la usuluhishi kufanyika pasipo kutumia mfumo wa kielektoniki na usuluhishi ulikuwa ukifanyika katika ofisi za mikoani na hivyo kufanya utaratibu wa ufuatiliaji kuchukua muda mrefu katika kutatua”. Amesema.