Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam CPA, Amos Makalla amepiga marufuku utaratibu wa wafanyabiashara kuuza bidhaa kwa kuzipanga chini hususani bidhaa za chakula.
RC Makalla ametoa onyo hilo wakati wa zoezi la usafi wa pamoja katika soko la Machinga complex mwishoni mwa wiki ambapo amewaelekeza viongozi wa masoko yote kudhibiti na kusimamia agizo Hilo.
Ameeleza kuwa kupanga bidhaa za vyakula chini ni hatari kiafya hasa msimu huu wa mvua ambapo kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Aidha, ametumia zoezi hilo kuwahakikishia wafanyabiashara waliokuwa katika soko la kariakoo kuwa ujenzi ukikamilika kipaumbele kitakuwa kwa wale waliokuwepo awali.
Pamoja na hayo, RC Makalla ameendelea kupiga marufuku ufanyaji biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa na kuwataka wafanyabiashara kwenda kwenye masoko rasmi Ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali hususani mikopo.
Ameelekeza kila mtendaji kwenye eneo lake kuhakikisha anasimamia zoezi la usafi na kubainisha kuwa watakaoonekana kulegalega watachukuliwa hatua.