Watu wengi hufikiri kuwa mafanikio hutokana na utafutaji wa fedha peke yake, jambo ambalo si kweli. Kuna mambo mengi zaidi yanayoweza kumfanya mtu afanikiwe mbali na kuwa mfanyakazi mahiri anayefanya kazi kwa bidii. Tabia, ni jambo moja wapo linaloweza kuchelewesha mafanikio au kufanya yawahi kukufikia. Mtindo wako wa maisha pia unaweza kufanya uwe zaidi ya mchapakazi na kutimiza malengo yako kirahisi zaidi.
Hizi ni baadhi ya tabia ambazo zinaweza kuchelewesha mafanikio yako;
Kutoa hadi zisizo na uhalisia: Ikiwa una tabia ya kutoa ahadi na kutozitimiza, tambua kuwa unaharibu picha ya kampuni/biashara yako na watu hawakuwa na imani kubwa na wewe kwa sababu utakuwa umewekwa katika kundi la watu wasio makini na hii inaweza kupelekea kupoteza ushirikiano kutoka kwa watu wenye mtandao mkubwa zaidi. Hakikisha unatoa ahadi unazoweza kutimiza ili kujenga uaminifu kwa watu (walio chini yako au juu yako). Ili kurahisisha hilo, andika ahadi katika kalenda yako ili uweze kukumbuka na kuifanyia kazi.
Kuweka malengo bila kuyafanyia kazi: Ni jambo la kawaida kusikia watu wana mipango madhubuti kabisa, lakini baada ya kipindi fulani ukiuliza maendeleo ya mipango hiyo wanakuwa hawana majibu. Hii inaweza kusababisha mtu akose fursa zaidi. Jitahidi kuongelea mambo ambayo una uhakika yapo ndani ya uwezo wako. Anza na malengo madogo/ya muda mfupi ili kuweza kufikia yale ya muda mrefu. Kumbuka, hakuna aliyewahi kufanikiwa kwa maneno pekee.
Kuwatupia malalamiko watu wengine: Siku zote mafanikio hutoka ndani kwa mtu binafsi, kwa kuwalalamikia watu wengine makosa kwa makosa tunayofanya, ni dhahiri kuwa tulikuwa tunasubiri watu wengine watutafutie mafanikio jambo lisilowezekana. Kubali makosa yako, jifunze kupitia makosa hayo ili kufanya vizuri zaidi na kutimiza malengo yako.
Kutojiamini: Mara nyingi, watu wenye ujasiri hufanikiwa, kwani waamini watafanikiwa kabla watu wengine hawajafanya hivyo. Kutokana na hilo inakuwa rahisi kwao kufanya kazi kwa bidii kwa imani kuwa watafanikiwa. Kujiamini humsaidia mtu kusonga mbele licha ya vikwazo ambavyo anaweza kuwa anakumbana navyo. Unapojiamini unapata nguvu ya kuendelea kupambana hata pale ambapo mambo yanakuwa magumu.
Kusubiria muda muafaka: Ifahamike kuwa hakuna muda sahihi wa kuanza ikiwa unataka kufanikiwa. Watu wengi ambao hulalamika kuwa hawafanikiwi mara nyingi huwa ni watu ambao wanasubiri wakati sahihi kupigania ndoto zao. Kila siku kuna fursa mpya ambazo zinasubiri kutekelezwa, kama kila mtu angesubiri muda muafaka ingekuwaje? Kwa kuweka uoga pembeni, ni dhahiri kuwa utatimiza malengo yako hivyo anza leo na hata kama utafeli usikikate tamaa, jaribu tena na tena.
Kukata tamaa: Vikwazo hutokea ili kumuandaa mtu kuelekea kwenye mafanikio. Hakuna mtu aliyefanikiwa ndani ya siku moja. Wote waliofanikiwa wamepitia vikwazo mbalimbali, waliambiwa hapana mara nyingi lakini hawakukata tamaa. Ikiwa unapitia wakati mgumu, tafuta njia za kusuluhisha vikwazo unavyonavyo ili kuweza kusonga mbele na kutimiza malengo yako.
Kupuuzia umuhimu wa kujifunza: Elimu haina mwisho, kila siku mambo mbalimbali yanavumbuliwa. Kama mtu makini anayetaka kutimiza malengo yake, ni muhimu kujifunza ili kwenda na wakati, kujua mambo mengi zaidi. Hakuna haja ya kwenda darasani, unaweza kujifunza kupitia vitabu, mikutano, semina na mtandao.
Pamoja na yote hayo, ni muhimu kuzingatia afya bora ili kufikia malengo yako. Kula vizuri, fanya mazoezi tembelea taasisi za afya ili kuangalia afya yako mara kwa mara. Pia weka muda wa kutosha kwa ajili ya kupumzika.