Wajasiliamali wadogo na wa kati kutoka Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameomba mafunzo na elimu zaidi kuhusu kuhifadhi mazao hasa zao la mchele. Akizungumza katika kampeni ya siku moja iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), mjasiliamali Elituliza Mmari amesema wanaiomba Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) pamoja na TBS kuwapa mafunzo kuhusu kutunza mazao yao hususani mchele.
Pamoja na hayo, Mmari ametaja mojawapo ya vikwazo wanavyokutana navyo wajasiliamali kuwa ni ukosefu wa eneo la uhakika kwa ajili ya kufanya shughuli zao na vilevile ukosefu wa elimu ya kutengeneza bidhaa za uhakika zinazofaa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano wa TBS, Neema Mtemvu , amesema Shirika hilo limekuwa likitoa elimu ya bure kuhusu umuhimu wa kuwa na bidhaa zilizodhibitishwa, na hivyo kuwataka wajasiliamali wa Kahama kujiunga kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ili nao waweze kupatiwa mafunzo hayo. Aidha Mtemvu pia ameeleza kuwa, TBS inategemea kufanya kampeni kwa wajasiliamali wadogo na wa kati mjini Tarime, Mara na Nyamagana mkoani Mwanza.