Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka vijana wabunifu na wavumbuzi wa programu mbalimbali za kidijitali kujitokeza kupata rasilimali zitakazowawezesha kupata fursa ya kutengeneza ajira; kujiletea kipato na kutatua changamoto mtambuka za jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari amesema mapema leo Jumatatu Novemba 14, 2022 kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine imeamua kuwafungulia milango muhimu vijana wabunifu katika Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwapa uwezeshaji uliokuwa unakwamisha ubunifu miaka yote nchini.
Amesema TCRA imeweka mazingira rafiki kwa vijana wabunifu wa TEHAMA kutengeneza fursa za kukuza ubunifu na hatimae kuzaa ajira kwa vijana wengine.
“Serikali imeamua kutoka rasilimali kwa vijana wabunifu katika sekta ya TEHAMA.
Rasilimali za mawasiliano zinazotolewa na TCRA kwa ajili ya vijana wabunifu kufanya majaribio ni pamoja na misimbo ya USSD, yaani rasilimali-namba. Hizi ni namba maalum zinazotumika kumpa mbunifu fursa ya kusambaza teknolojia aliyoibuni ndani na nje ya nchi. Pia TCRA kwa sasa wanato kikoa (domain) cha dot tz (.tz) na masafa ya mawasiliano.”
Ameeleza kuwa“fursa zilizotolewa zinahitaji kijana kuwa na ubunifu kama mtaji wake na vifaa vya gharama nafuu vya TEHAMA kama vile kompyuta mpakato na simu ya kiganjani au vifaa rununu pendwa kama vile kishikwambi kukamilisha ubunifu wake.
Tumejipanga kuhakikisha wabunifu wapya hasa wa sekta ya TEHAMA wanaoweza kutatua changamoto za jamii yetu wanapata rasilimali hizi za mawasiliano, ili washiriki katika uchumi wa kidijiti.”
Amefafanua kuwa “tuna utaratibu wa kutoa rasilimali hizi kwa muda wa miezi mitatu; ambazo tunatoa [kwa mbunifu] baada ya kuidhinishwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo hujiridhisha kubaini kama wazo la kibunifu linakidhi kufanyiwa majaribio na hapo ndipo tunatoa rasilimali za masafa au misimbo ya namba fupi kwa muda wa majaribio wa miezi mitatu.
“Ni wazi kwamba gharama ya rasilimali za Mawasiliano ni kubwa, kiasi kwamba mbunifu au mjasiriamali wa TEHAMA anaechipukia, mathalani mwanafunzi aliyehitimu au aliyepo kwenye mafunzoni, anapohitaji kufanya majaribio ya ubunifu wake wa TEHAMA hataweza kumudu gharama za rasilimali hizo kama vile masafa, kikoa au rasilimali namba, maarufu kama misimbo ya USSD au wengine huita misimbo ya namba fupi,” amesema Dk. Jabir.
Mbali na fursa zinazotolewa na TCRA, COSTECH na Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa wabunifu wa TEHAMA nchini, Tume ya TEHAMA (ICTC) nayo haipo nyuma.
Tume hiyo inaendesha program ijulikanayo kama Softcentre inayotoa msaada wa moja kwa moja kwa kampuni changa (Startups), ikiwa ni kutekeleza mpango wa mapinduzi ya kidijitali unaolenga kutatua tatizo la ajira na kukuza ubunifu wenye tija.
Pia imekuwa ikiendesha Tuzo za kampuni changa (ICT Startups Awards) zinazotumia TEHAMA kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwa bunifu zenye tija.
Mashindano kwa kampuni changa yanaendeshwa na Tume ya TEHAMA kwa malengo ya kutambua wabunifu nchini na kuwawezesha.
Moja ya Malengo ya Kimkakati ya TCRA ni Kukuza Ubunifu, uzalishaji wa maudhui ya ndani na ujanibishaji (localization).
Katika kulitambua hilo, TCRA huratibu vikao vya mashauriano na wadau wakuu wanaojishughulisha na ubunifu kujadili masuala yanayohusu fursa na changamoto za programu za ubunifu wa TEHAMA kukua na jinsi TCRA inavyoweza kuweka mazingira wezeshi ikizingatiwa kwamba Mamlaka hiyo ni taasisi wezeshi katika sekta pana ya Mawasiliano.
Utoaji wa Rasilimali za Mawasiliano ili kukuza ubunifu na utafiti katika TEHAMA, unabainisha kuwa TCRA imedhamiria kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu wanaotaka kutumia rasilimali za mawasiliano kufanya majaribio ya mawazo mbalimbali ya ubunifu/utafiti.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeondoa malipo ya ada ya maombi na usajili wa leseni wa rasilimali hizo kwa ajili ya wabunifu wenye nia ya kubuni suala lolote litakalorahisisha mazingira ya kawaida ya kila siku ya mwananchi.
Pia, watoa huduma za mawasiliano ya simu kwa kuwaunganisha wabunifu hawa bure kwenye mitandao yao wakati wa kipindi cha majaribio.
Wabunifu wanaotaka kutumia fursa hii wanaweza kuwasiliana na Dawati la Huduma la TCRA kupitia namba 0800008272 au kutembelea tovuti www.tcra.go.tz